Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

WAANDISHI NA WABUNIFU WATAKIWA KUTUMIA KAZI ZAO KUWA FURSA ZA BIASHARA


Serikali imewataka Waandishi na Wabunifu wa kazi za fasihi kutumia kazi zao kuwa ni fursa za uchumi
Kwani kazi hizo l si utamaduni pekee, bali ni mali miliki zenye thamani kubwa ya kiuchumi zinazoweza kuzalisha ajira, mapato, na fursa za biashara kwa waandishi, wachapishaji, na wadau wote katika mnyororo wa thamani.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dennis Londo (Mb) wakati wa hafla ya ufungaji wa Maonesho ya Uchumi wa Ubunifu wa Mashariki 2026.( Mashariki Creative Economy Expo 2026), Agosti 21,2026 katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.

Londo amesema Vitabu, riwaya, na mashairi vina uwezo wa kubadilishwa kuwa maudhui ya filamu, michezo ya kuigiza, na machapisho ya kidijitali ili kufikia masoko ya ndani, kikanda, na kimataifa.

Aidha amesema Mafanikio ya matukio kama Mashariki Creative Economy Expo 2026 hayatapimwa kwa mijadala pekee, bali kwa idadi ya miradi, ushirikiano wa kibiashara, na ajira zitakazozalishwa kwa ajili ya wabunifu.

Naibu Waziri Londo amesema Serikali inaweka mazingira wezeshi ya kibiashara kwa kuimarisha mifumo ya hakimiliki, ili kuwezesha wabunifu kutumia taaluma zao kama chanzo rasmi cha kipato na uwekezaji pamoja na kushirikiana na wadau ili kuhakikisha kazi za ubunifu za Watanzania zinatambuliwa, zinalindwa, na kupata masoko mapana ya ndani na kimataifa.

Vilevile amesema kuna haja ya kuwajengea uwezo waandishi kuelewa thamani ya kazi zao, huku taasisi za fedha na wawekezaji wakihimizwa kuanza kuangalia mali miliki kama sehemu halisi ya uchumi wa maarifa unaostahili mikopo na mitaji.

Ameongeza kuwa ni lazima kuwepo kwa ushirikiano wa kibiashara kati ya waandishi, watayarishaji wa filamu, na wawekezaji ili kuongeza thamani ya simulizi za Kitanzania na Kiafrika katika masoko ya kimataifa.