Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah ameshiriki Mkutano wa 46 Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha Novemba 25, 2024 ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa 46 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo unaotarajiwa kufanyika Novemba 28, 2024
Mkutano huo umepitia na kujadili taarifa mbalimbali zilizowasilishwa kwao na timu ya Wataalam waliokutana jijini hapa kuanzia tarehe 22 - 24 Novemba 2024.
Taarifa zilizowasilishwa na kujadiliwa na Makatibu Wakuu ni pamoja na Taarifa ya utekelezaji wa maamuzi ya awali ya Baraza la Mawaziri; Taarifa ya Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; Taarifa kuhusu masuala Forodha, Biashara na masuala ya kifedha; Taarifa kuhusu Miundombinu, Sekta za Uzalishaji, Sekta za Kijamii na masuala ya Kisiasa; Taarifa kuhusu masuala Fedha na Taarifa kuhusu Taasisi za Jumuiya.
Akifungua Mkutano huo, Mwenyekiti ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Sudan Kusini, Mhe. Beny Gideon Mabor amewakaribisha wajumbe kwenye Mkutano huo na kuwaomba kuchangia kwa hoja agenda zote zilizowasilishwa kwao ili kufikia makubaliano ya pamoja kwa maslahi mapana ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ni kuziimarisha Nchi Wanachama na Wananchi wake katika sekta za Uchumi, Siasa na Jamii.
Viongozi wengine kutoka Tanzania walioshiriki Mkutano huo ni Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Eliakim Chacha Maswi, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk. Tausi Kida, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Bw. Elijah Mwandubya pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini.