Habari
Maduka yaliyopo Ubungo Trade Center, Dar es Salaam, yamenunuliwa huku asilimia 90 ya maduka hayo yakimilikiwa na Watanzania.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt.Selemani Jafo (Mb) amesema asilimia 70 ya maduka yaliyopo Ubungo Trade Center, Dar es Salaam, yamenunuliwa huku asilimia 90 ya maduka hayo yakimilikiwa na Watanzania.
Ameyasema hayo alipotembelea kuona maendeleo ya ujenzi wa Kituo Kikubwa cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC - East Africa Commercial and Logistic Centre) kilichopo Ubungo Dar es Salaam Januari 07,2025.
Dkt. Jafo amesema kuwa eneo hilo ni muhimu kwa nchi kwani kukamilika kwake kutaongeza tija na manufaa katika ukuaji wa uchumi na kuongeza kuwa Watanzania wameanza kuchangamkia fursa hiyo kwa kuanza kumiliki maduka na wanatarajia ajira za moja kwa moja zaidi ya 15,000 na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 50,000.
Dkt.Jafo pia amefafanua kuwa ndani ya mwaka 2025 kazi ya ujenzi itakamilika na maduka hayo yataanza kutumika hivyo Taifa linajivunia kuwa limepata eneo la uwekezaji na biashara ambapo Afrika Mashariki na Kati itakuwa soko kubwa zaidi.
Aidha Dkt.Jafo amesema eneo hilo ni muhimu kwa sababu usafiri unafikika kwa urahisi kwani lipo kwenye makutano ya Barabara ya Nelson Mandela na Morogoro, ni kilomita 10 kutoka bandarini, kilomita nane kutoka stesheni ya reli na kilomita 14 kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. (JNIA).
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa EACLC, Bi. Cathy Wang amesema dhamira ya mradi huo ni kuleta bidhaa zenye ubora wa juu kwa bei nafuu na kusema kuwa eneo hilo litakuwa na sehemu ya kuegesha magari ambayo yatabeba zaidi ya magari 1,000 kwa wakati mmoja na kutakuwa na huduma ya saa 24 kwani mifumo ya ufuatiliaji na doria itajengwa ndani ya eneo hilo.
Ameongeza kuwa ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 95 na ukikamilika kitakuwa utakiwa na maduka 2600 na litakuwa ni daraja linalounganisha wafanyabiashara wa Tanzania na China pamoja na kuwavutia wafanyabiashara kutoka nchi nyingine za Afrika Mashariki kununua bidhaa Tanzania na litakuwa soko la kwanza la kimataifa katika ukanda wa Afrika Mashariki ambalo litahusisha uuzaji wa bidhaa mbalimbali kama soko la Guangzhou.