Habari
Makamu wa Makamu Rais CUBA atembelee Kiwanda cha Viuadudu cha Kibaha

Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Valdes Mesa amesema Serikali ya Cuba itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha kiwanda cha kuzalisha Viuadudu vya kuua Viluwiluwi vya Mbu wanaoeneza Malaria kilichopo Kibaha mkoani Pwani ili kiendelee kuhudumia Watanzania na nchi nyingine za Afrika.
Mhe. Mesa ametoa kauli hiyo alipotembelea Kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 23 hadi 25 Januari 2024.
Amesema nchi yake itaendelea kutoa msaada wa kitaalam kwa mamlaka za Tanzania ili kukiwezesha kiwanda hicho kuzalisha bidhaa tofautitouti mbali na viuadudu vya malaria zikiwemo mbolea, viuatilifu na bidhaa nyingine za kilimo
Pia amesema kiwanda hicho kitaendelea kuwa mfano wa ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya Tanzania na Cuba katika sekta mbalimbali ikiwemo ya afya.
“Nimepata bahati ya kukitembelea kiwanda hiki kwa mara ya pili sasa, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2016 wakati kinakamilishwa. Napongeza hatua iliyofikiwa kwenye uzalishaji” amesema Mhe. Mesa.
Amesema kiwanda hicho kinatakiwa kutunzwa kwani ni chanzo cha ajira kwa watanzania lakini pia kinakuza uchumi wa Tanzania na kanda kwa ujumla kwa kuimarisha afya za watanzania na watu wa nchi jirani ambao wanasumbuliwa na ugonjwa wa malaria.
Awali akizungumza kumkaribisha Mhe. Mesa katika kiwanda hicho, Mkuu wa Mkoa wa Pwani , Mhe. Abubakar Kunenge amesema kuwa anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhamasisha uwekezaji wa viwanda kwenye mkoa huo na kuwakaribisha wawekezaji zaidi kutoka Cuba kuwekeza.
Miongoni mwaViongozi wengine walioshiriki ziara ya Mhe. Mesa kwenye kiwanda hicho ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki, Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Humphrey Polepole na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Yordenis Despaigne Vera.