Habari
MHE. KIGAHE: MAZINGIRA YA KUFANYA BIASHARA YANAENDELEA KUBORESHWA
Serikali ya Tanzania imeahidi kuendelea kuboresha mazingira rafiki ya kufanya biashara na kuwaalika wawekezaji kutoka Afrika na duniani kwa ujumla kuja kuwekeza.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe wakati wa uwekwaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha mbolea cha Itracom kinachojengewa na wawekezaji kutoka Burundi.
Hafla hiyo iliyoongozwa na Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye ilifanyika katika eneo la Nala nje kidogo ya jiji la Dodoma ambapo pia viongozi mbalimbali kutoka Tanzania na Burundi walihudhuria.
Naibu Waziri Kigahe alisema kuwa uwekezaji wa kiwanda hicho ni matokeo ya urafiki wa muda mrefu wan chi hizo na kuwa kiwanda hicho kinaenda kuwasaidia Watanzania ambao zaidi ya asilimia 65 wamejiajiri katika sekta ya kilimo.
“Tunafarajika sana kwa uwekezaji huu katika sekta ya viwanda. Mbolea ni kitu muhimu sana kwa watanzania. Sasa hivi tunatumia zaidi ya tani laki saba kwa mwaka na kiwanda kiwanda hiki kinaenda kuzalisha tani laki sita. Huu ni uwekezaji mzuri na tunawashukuru sana ndugu zetu wa Burundi kwa uwekezaji huu.” Alisema Naibu Waziri huyo.
Alisema pia matokeo ya uwekezaji wa kiwanda hiko utaenda kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao mbalimbali na kuhahakikishia nchi uhakika wa chakula.