Habari
WAZIRI JAFO AFURAHISHWA NA UWEKEZAJI KIWANDA CHA MAGODORO YA DODOM ASILI, ATAKA WALIFIKIE SOKO LA AFRIKA.
WAZIRI JAFO AFURAHISHWA NA UWEKEZAJI KIWANDA CHA MAGODORO YA DODOM ASILI, ATAKA WALIFIKIE SOKO LA AFRIKA.
Waziri wa Viwanda na Biashara,Mhe.Dkt.Selemani Jafo (Mb) amewataka Wamiliki wa Kiwanda Cha Magodoro ya Dodoma Asili kuhakikisha wanalifikia Soko huru la Afrika (AfCFTA) katika uuzaji wa magodoro huku akifurahishwa na jinsi ambavyo wametoa ajira kwa Watanzania pamoja na kukuza uchumi wa Nchi.
Mhe. Dkt.Jafo ameyasema hayo wakati wa ziara ya kutembelea kiwanda hicho kwa lengo la kujionea shughuli za uzalishaji, changamoto na kusikiliza maoni na ushauri wa kuboresha Aprili 10, 2025 jijini Dodoma.
Waziri Jafo amesema anafarijika kuona uwekezaji mkubwa ambao umefanywa ambapo zaidi ya watumishi 130 wameajiriwa ambapo amesema jambo hilo lina tija kwa Nchi.
Kiwanda hicho kinalipa kodi ya zaidi ya Sh bilioni 3 kwa mwaka, hivyo kuongeza tija katika uchumi wa Nchi.
Mhe. Jafo ameongeza kuwa amefarijika kwa kuona namna ambavyo Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linavyosimamia Viwango na kutoa ushirikiano katika Kiwanda hicho.
"Nikiwa Waziri napata faraja kuona kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inaenda vizuri.Niwaombe wawekezaji kuongeza spidi katika uzalishaji ili ikiwezekana kulifikia soko la Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
"Imani yetu tutaendelea kupambana kuhakikisha tunaendeleza uchumi wetu. Nimefarijiika kuna hata kinadada wengi wamepata ajira hapa ,"amesema Waziri Jafo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma,Bi.Mwajabu Nyamkomola amewapongeza wawekezaji wa Kiwanda hicho kwa kuweza kutoa ajira kwa watanzania ikiwemo na wanawake.
Kwa upande wake mfanyakazi wa Kiwanda hicho, Tausi Mayonga amesema amefanya kazi kwa muda wa miaka 13 ambapo amemshukuru mwajiri wao kwa kutoa usawa katika suala la ajira.