Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

WAZIRI JAFO APONGEZA CLOUDS MEDIA KWA KUPELEKA WAFANYABIASHARA KUJIFUNZA CHINA


Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt Selemani Jafo, ameipongeza Clouds Media kwa kuanzisha programu ya kupeleka Wafanyabiashara wa Tanzania, nchini China kwa lengo la kujifunza mbinu za biashara na kupata ujuzi wa kimataifa.

Akizungumza na wafanyabiashara hao Septemba 17, 2025 katika Viwanja vya Ndege vya Kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA), Dkt Jafo alisema kuwa safari hiyo imelenga kupanua fikra na wigo wa biashara kwa Wafanyabiashara hao, ili waweze kufanya mambo makubwa zaidi kuliko walivyokuwa wakifanya hapo awali.

Aidha, Dkt Jafo alisisitiza kuwa safari hiyo ni hatua muhimu katika kupanua mtazamo wa wafanyabiashara na kuwapa ujuzi unaoendana na ushindani wa kimataifa kutoka kwa taifa lenye mafanikio makubwa ya kibiashara kama China

Aidha, Waziri Jafo alisema kupitia programu hiyo, Serikali inahamasisha wafanyabiashara kufanya biashara kwa unadhifu na kutumia teknolojia mpya, hasa katika sekta kama uundaji wa fanicha, ambapo ubora wa bidhaa unahitaji kuimarishwa hasa upande wa umaliziaji (finishing) ili kushindana na bidhaa za nje.

“Juhudi hizi ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kuhakikisha biashara za Kitanzania zinakua na kuleta maendeleo endelevu ya kiuchumi,” amesema Dkt Jafo.

Aidha aliahidi kuwa serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za Clouds Media na wadau wengine katika kupeleka wafanyabiashara zaidi nje ya nchi kwa ajili ya mafunzo, kwa lengo la kuwawezesha kuwa mabalozi wa mabadiliko ya kiuchumi na Maendeleo ya Taifa.

Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Clouds Media Group, Bi Sheba Kussaga, alisema safari hiyo ilihusisha wafanyabiashara zaidi ya 50, wengi wao wanawake, ililenga kutoa mafunzo ya moja kwa moja kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa na kuwapatia washiriki mtazamo wa kimataifa kuhusu biashara ambapo walitembelea miji mikubwa ya kibiashara China ikiwemo Guangzhou, Yiwu, na Foshan.

Nao Wafanyabiashara walikuwa katika Safari hii akiwemo Bi, Happiness Nyalugenzi na Bw.Bakari Nzagamba wamesema walipata mafunzo mbalimbali kuhusu upanuzi wa masoko, uwezeshaji wa kifedha, na kujenga mitandao ya ushawishi wa kibiashara.