Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Dkt.Jafo ataka watanzania kununua mabati yanayozalishwa nchini


DKT.JAFO ATAKA WATANZANIA KUNUNUA MABATI YANAYOZALISHWA NCHINI

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo(Mb) amesema Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kuvilinda Viwanda vya mabati nchini kwa kuweka kodi kubwa kwa mabati yanayotoka nje ya Nchi huku akiwataka Watanzania kununua mabati yanayozalishwa na Viwanda nchini.

Dkt.Jafo ameyasema hayo leo Aprili 22,2025, mara baada ya ziara ya kukagua shughuli za uzalishaji wa Kiwanda cha mabati Cha ALAF Jijini Dodoma ambapo amesema kuwa kiwanda hicho uzalishaji wake umekuwa ukiongezeka kila siku.

Waziri Jafo amesema Kiwanda hicho ni cha kihistoria kwani kipo nchini tangu mwaka 1960 na kina share na Serikali kwa asilimia 24.

Amesema Kiwanda hicho kwa sasa kinauwezo wa kuzalisha bati ya rangi nyeupe tani 100,000 na za rangi tani 75,000 kuanzia geji 22 hadi 32 kulingana na mahitaji husika hali inayochangia nchi kujitosheleza kwa bidhaa hiyo ya mabati.

"Maana yake tuna kila sababu ya kuweka mikakati ya kuzuia uingizaji wa mabati kutoka nje ili kulinda ajira zetu,"amesema Waziri Jafo

Amesema wanapoenda katika mchakato wa bajeti lazima waangalie mikakati ya bati kutoka nje kwa kuweka kodi ya kutosha ili ya ndani yaweze kuzalishwa na kupata soko

"Kwa sababu lazima tuvilinde Viwanda vya ndani.Nafahamu mmeajiri zaidi ya watu 500, niwahakikishie Serikali itaendelea kuwalinda ila niwaombe Watanzania tununue bati za ndani,"amesema Waziri Jafo.

Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi,Sekta ya uwekezaji Viwanda na Biashara Jiji la Dodoma. Bi.Mwajabu Nyamkomola ameziomba Halmashauri zote nchini kutumia mabati ya Alaf katika ujenzi wa vitu mbalimbali ikiwemo Zahanati na vituo vya Afya.


"Tumeona ubora wa vitu vilivyozungumzwa wakiwepo TBS wanahakikisha wanapata bidhaa zenye ubora wa hali ya juu na utaendelea kuhakikisha hivi Viwanda havipati vikwazo vyovyote bali wanazidi kusonga mbele ,"amesema Bi. Nyamkomola

Naye Meneja Uhusiano wa ALAF Bi.Hawa Bayumi,amesema katika kipindi cha mwaka mmoja Alaf inazalisha bati za rangi hapa hapa nchini na wanauwezo wa kuhudumia wateja wao kwa wakati katika Viwango na ubora unaokubalika.