Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

WAZIRI KAPINGA ASHIRIKI MAJADILIANO YA BIASHARA NA UWEKEZAJI KATI YA TANZANIA NA DANGOTE GROUP


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga(Mb), Agosti 07, 2026, ameambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe.Prof. Kitila Mkumbo (Mb), pamoja na Mawaziri wa sekta mbalimbali na Wakuu wa Taasisi za Serikali, katika ziara ya kutembelea viwanda na miradi mbalimbali ya Dangote jijini Lagos, Nigeria.

Katika ziara hiyo, ujumbe wa Serikali ya Tanzania umkutana na uongozi wa Dangote Group na kujadili fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji nchini Tanzania, ikiwemo Mradi wa Bandari ya Bagamoyo na Kongani ya Viwanda, uzalishaji wa mbolea pamoja na uzalishaji wa umeme kwa kutumia makaa ya mawe.

Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais wa Dangote Group, DVG Edwin, ametaka kufahamu mifumo na haki zinazopatikana kwa wawekezaji nchini Tanzania, hususan katika masuala ya ardhi, madini na uzalishaji wa umeme.

Akijibu hoja hizo, Prof. Mkumbo amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum Tanzania (TISEZA), pamoja na Wakuu wa Taasisi walioshiriki ziara hiyo chini ya sekta husika na timu ya kiufundi, kukutana na uongozi wa Dangote Group na kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu masuala hayo.

Hatua hiyo inalenga kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Dangote Group.