Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

WAZIRI KAPINGA ATOA RAI KWA WATUMISHI KUFANYA KAZI KWA USHIRIKIANO, UPENDO, WELEDI NA UAMINIFU


Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga ametoa rai kwa Watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa weledi, uaminifu upendo na ushirikiano ili sekta hiyo iendelee kuchangia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Rai hiyo ameitoa Februari 11, 2026 Mtumba, jijini Dodoma wakati wa mapokezi ya Katibu Mkuu, Balozi Waziri Salum na Naibu Katibu Mkuu, Bw. Aristides Mbwasi walioteuliwa hivi karibuni na Rais na kuapishwa kushika nyadhifa hizo pamoja na makabidhiano ya Ofisi ya Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu.

Akiongea na Watumishi wa Wizara hiyo , Waziri Kapinga amewasisitiza Watumishi hao umuhimu wa umoja, upendo na ushirikiano miongoni mwa Watumishi wa Wizara hiyo pamoja na Taasisi zilizo chini yake, akiwataka kuwapa Viongozi wao ushirikiano wa kutosha ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kufikia Malengo ya Dira ya Taifa 2050.

Amesema mafanikio ya Wizara yanategemea mshikamano, uwajibikaji na utendaji kazi wenye kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhe Balozi Waziri Salum amewasisitiza Watumishi hao pia kufanya kazi kwa bidii, weledi na utu katika utoaji huduma kwa Wafanyabiashara na Wananchi kwa ujumla ili kuijenga wizara hiyo.

Amewataka watumishi kuwajibika kikamilifu na kuhakikisha kuwa Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri Mhe Judith Kapinga wanang’ara kupitia mafanikio ya sekta ya viwanda na biashara katika kuongeza Ajira, na kukuza uchumi wa Viwanda shindani.

“Nimekuja wizarani kumsaidia Waziri ili muweze kufanya kazi kwa weledi mkubwa. Nawategemea sana, nimekuja kuleta nguvu; sina miujiza maana miujiza ipo hapa.

Aidha, Ameongeza kuwa ana imani kubwa na Watumishi hao na kusisitiza umuhimu wa kujenga uaminifu wa pande zote ili kufanikisha malengo ya pamoja.

Kadhalika, Naibu Katibu Mkuu, Aristides Mbwasi atatoa ushirikiano kwa Viongozi na Watumishi wa Wizara hiyo ili kuhakikisha sekta ya viwanda na biashara inaendelea kukua na kuchangia ipasavyo katika uchumi wa taifa