Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA, CTI KUIMARISHA USHIRIKIANO KUKUZA SEKTA YA VIWANDA


📌 Uongozi mpya wa CTI ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Frank Dafa, wajitambulisha kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara.

📌 Serikali yasistiza umuhimu wa mahusiano imara na sekta binafsi katika kukuza uwekezaji na uzalishaji viwandani.

📌 CTI yaeleza dhamira ya kuendeleza ushirikiano na Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara na maendeleo ya viwanda.

DAR ES SALAAM

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Rajab Salum, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mahusiano na ushirikiano kati ya Wizara na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (Confederation of Tanzania Industries – CTI) katika kuendeleza sekta ya viwanda nchini.

Katibu Mkuu ameyasema hayo Novemba 11,2026 jijini Dar-es-salaam wakati wa kikao na uongozi wa CTI ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa sasa wa shirikisho hilo, Frank Dafa, pamoja na Eng. Leodegar Tenga, Mkurugenzi Mtendaji aliyemaliza muda wake, kilicholenga kujitambulisha kwa uongozi wa Wizara na kujenga mahusiano ya kikazi.

Katika kikao hicho, Katibu Mkuu ameeleza kuwa Serikali inatambua nafasi ya sekta binafsi katika kukuza uchumi na kuimarisha uzalishaji wa viwandani, hivyo ni muhimu kuendeleza mazingira mazuri ya ushirikiano yatakayowezesha Serikali na wawekezaji kufanya kazi kwa pamoja.

Amesisitiza kuwa mahusiano mazuri kati ya Serikali na wenye viwanda ni muhimu katika kuboresha mazingira ya uwekezaji, kusikiliza changamoto za wazalishaji na kuhakikisha sekta ya viwanda inaendelea kutoa mchango wake katika maendeleo ya taifa. Aidha, ameeleza kuwa Wizara itaendelea kuwa karibu na CTI pamoja na wadau wengine kwa kusikiliza maoni yao, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mawasiliano katika masuala mbalimbali ya maendeleo ya sekta hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CTI, Frank Dafa, ameishukuru Wizara kwa ushirikiano unaoendelea kujengwa na kueleza dhamira ya shirikisho hilo kuendeleza mahusiano mazuri na Serikali katika kuwakilisha maslahi ya wanachama wake na kuchangia maendeleo ya sekta ya viwanda.

Naye Eng. Leodegar Tenga amesema uongozi wa CTI utaendelea kushirikiana na Wizara katika kutoa maoni, kuwasilisha mitazamo ya wazalishaji na kushiriki katika mijadala mbalimbali inayolenga kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. Kikao hicho ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mahusiano ya kikazi kati ya Wizara na CTI katika kukuza sekta ya viwanda nchini.