Habari
WAZIRI KAPINGA AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI WAZAWA KUCHANGAMKIA FURSA SEKTA YA VIWANDA
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), amewakaribisha wawekezaji wazawa nchini kuchangamkia fursa katika sekta ya viwanda, akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imerahisisha mazingira ya Biashara ili kukuza uwekezaji wa ndani.
Kapinga ameyasema hayo Aprili 24, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizindua bidhaa nne za chapa ya Riviera.
Aidha, Waziri Kapinga amesema Serikali haitofungia Biashara zinazojitokeza, bali itazielekeza kufuata taratibu ili kulinda afya ya umma.
Waziri Kapinga amempongeza Mkurugenzi wa Lomatan, Bi. Loveness Edwin Mamuya kwa ujasiri wa kuingia kwenye sekta ya vinywaji vikali ambavyo vina ushindani mkubwa.
Ameongeza kuwa uwekezaji huo unathibitisha kuwa Watanzania wana uwezo wa kuwekeza kwenye sekta yoyote.
Kapinga amemhakikishia Loveness kuwa Wizara yake itakuwa pamoja naye kutatua changamoto zozote zitakazojitokeza ili kuhakikisha Biashara hiyo inastawi na kuingiza mapato kwa mwekezaji na Serikali.
Amesisitiza kuwa kupitia Tume ya Ushindani (FCC), Serikali itaendelea kupambana na vinywaji haramu na vile ambavyo havijathibitishwa ubora ili kulinda soko la bidhaa halali.
“Tunaendelea kuwasisitiza na wengine ambao wanataka kuingia kwenye hii sekta, tumerahisisha mazingira ya kufanya biashara, siku hizi hatufungii biashara. Una kinywaji chako hakina uthibitisho, sisi hatukufungii bali tunakuelekeza namna ya kufanya ili kulinda afya ya Watanzania. Kwa hiyo tunawatia moyo wale wengine ambao wako kwenye sekta wafanye kama dada Loveness”, ameeleeza Kapinga.
Bidhaa nne zilizoingizwa sokoni na Lomatan kwa brandi ya Riviera ni Jagaboom, Lomatan Whiskey, Lomatan Gin na Lomatan Vodka
