Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo(Mb) amesema kuwa Serikali kupitia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani (WRRB) imeunda Timu Maalum ili kutoa elimu kuhusu mfumo huo kwa wakulima ili kuondo changamoto katika mikoa ya Singida,Dodoma na Manyara.
Dkt.Jafo amebainisha hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini Mhe.Abeid Ighondo Ramadhani aliyetaka kufahamu Mkakati wa Serikali kutoa elimu ya mfumo huo kwa wakulima ili kuondoa changamoto katika Bunge la 12, Kikao cha 19 Mkutano wa 42, Juni 09,2025 Bungeni Jijini Dodoma.
Dkt.Jafo amesema Elimu kuhusu Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ilitolewa na itaendelea kutolewa katika ngazi ya Halmashauri na Kata zote nchini zinazozalisha mazao mbalimbali ikiwemo dengu na mbaazi katika mkoa wa Singida, ikiwemo Jimbo la Singida Kaskazini katika Kata za Mwasauya na Msange na zoezi la utoaji wa elimu kuhusu matumizi ya Mfumo huo ni endelevu.
Aidha Dkt.Jafo amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Stakabadhi Ghalani Bw.Asangye Bangu kufuatilia na kumpa mrejesho juu ya Malipo yanayocheleweshwa ma AMCOS hasa maeneo ya Singida ili wakulima wapate haki zao pamoja na kuhakikisha Maghala yote yakiwemo ya watu binafsi yanasajiliwa kwenye mfumo huo mapema.