Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Waziri wa Viwanda na Biashara Aagiza Hatua Kuchukuliwa Dhidi ya Msongamano wa Magari Eneo la Viwanda Chang'ombe


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo(Mb) ameiagiza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha wanafanya utafiti wa kina katika eneo la Chang’ombe la Viwanda na kujua nini kifanyike kuondoa tatizo la msongamano wa Malori katika maeneo hayo.

Dkt.Jafo amesema anatambua kazi kubwa inayofanywa na Mkoa huo katika kuondoa changamoto ya foleni ni imani yake kuwa watapitia katika eneo hilo ili kubaini tatizo na kulifanyia kazi.

Dkt.Jafo amesema hayo wakati wa Ziara yake katika Kiwanda cha Cello kinachotengeneza vifaa vya plastiki vya majumbani na Maofisini kwa lengo la kuona na kusikiliza changamoto zinazowakabili ili kuzifanyia kazi, Chang’ombe jijini Dar es Salaam Julai 16,2025.

Aidha Waziri Jafo ameliagiza Baraza la Usimamizi na uhifadhi wa Mazingira (NEMC) kupitia maeneo hayo kuangalia Bohari za Makontena (ICD) ili kuona kama zina vyeti vya tathmini ya athari za kimazingira na itakapobainika ICD hizo zimejengwa nje ya utaratibu ziweze kuondolewa haraka ili kuruhusu shughuli za viwanda ziendelee kufanya kazi kama inavyotarajiwa chini ya Serikali ya awamu ya sita ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wa Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Ndg.Thabit Massa amesema kuwa wamepokea changamoto hiyo kubwa hasa msongamano wa Malori hivyo kutokana na maelekezo ya waziri kama Mkoa utaanza kujipanga kulifanyia kazi suala hilo mara moja.

Nae Mwakilishi wa Kiwanda hicho Bw. Vejay Soman amemshukuru Waziri Jafo kwa hatua zake za haraka za kufika Kiwandani hapo kusikiliza na kuona changamoto zinazowakabili na kuanza kuzifanyia kazi.