Habari
VIWANDA NA BIASHARA YAWAAGA WANAMICHEZO WANAOSHIRIKI SHIMIWI
📌Waagwa rasmi na Katibu Mkuu Viwanda tayari kushiriki mashindano hayo mkoani Kilimanjaro;
📌Waaswa kuwa na nidhamu kama watumishi wa umma na kuleta makombe.
Na Yasin Chaula
Wanamichezo wa Wizara ya Viwanda na Biashara wametakiwa kushindana kwa nidhamu na Kujituma ili kutwaa makombe, huku wakizingatia miongozo ya Utumishi wa Umma kwenye mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI).
​Wito huo umetolewa Septemba 18, 2026 Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jasiriamali Ndogo na za Kati, Mha. Simioni Irege, alipokuwa akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Waziri Salum, katika hafla ya kuwaaga wanamichezo hao wanaotarajiwa kuondoka Tarehe 19, Septemba 2026 kuelekea Mkoani Kilimanjaro ambako mashindano hayo yatafanyika.
​Mha. Irege amesema kuwa uongozi wa Wizara una imani kubwa na wawakilishi hao, hivyo ni vyema wakaendelea kubeba na kuonesha taswira nzuri ya Wizara na viongozi wake wakati wote watakapokuwa kwenye mashindano hayo.
​Akiwasilisha taarifa ya maandalizi, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bw. Said Msabimana, ameeleza kuwa wanamichezo hao wamefanya mazoezi ya kutosha kwa takribani miezi miwili kujiweka tayari kwa michuano hiyo.
​Mashindano ya SHIMIWI hufanyika kila mwaka yakilenga kujenga afya, kudumisha ushirikiano, na kuongeza ufanisi kazini miongoni mwa watumishi wa umma kupitia michezo mbalimbali ikiwemo soka, netiboli, riadha, kuvuta kamba, na michezo ya jadi.
