Habari
MITAALA IZINGATIE MABADILIKO YA KIUCHUMI NA TEKNOLOJI-A
MITAALA IZINGATIE MABADILIKO YA KIUCHUMI NA TEKNOLOJI-MAJALIWA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) ameagiza kuwa mitaala inayoandaliwa ihakikishe inazingatia mabadiliko ya kiuchumi na maendeleo ya teknolojia katika kuboresha elimu ya biashara kwa kutumia jukwaa la mtandao kutoa mafunzo ya biashara, matumizi ya programu za kisasa za biashara, na kupanua matumizi ya teknolojia katika biashara na ujasiriamali. “Hivyo, nitoe rai kwa taasisi za elimu na mafunzo ya biashara kujikita katika matumizi ya teknolojia katika utoaji wa mafunzo”
Amesema hayo leo (Ijumaa, Novemba 22, 2024) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa kongamano la tano la Maendeleo ya Biashara na Uchumi linalifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hazina jijini Dodoma.
Pia, ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na wadau waendelee kuimarisha na kuboresha mifumo ya elimu ya biashara katika ngazi zote za shule na vyuo na kuhakikisha inakidhi mahitaji ya soko la ajira.
Katika Hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka Taasisi za elimu na mafunzo ya biashara zihakikishe zinakuza ushirikiano na sekta binafsi ili kusaidia katika kubaini mahitaji halisi ya soko na kutoa mafunzo na elimu inayoendana na mabadiliko ya sekta ya biashara.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema ni muhimu kuhakikisha kuwa biashara si tu zinanufaisha wamiliki, bali pia zinachangia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. “Biashara zinapaswa kuchangia katika kulinda mazingira na ustawi wa jamii”.
Mhe. Majaliwa pia amewataka wadau wote wakiwemo Taasisi za Serikali, Taasisi za kifedha, na wadau wa maendeleo kuungana ili kuwezesha kutoa huduma za kifedha kwa wajasiriamali.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu ya maadili ya biashara, uwazi, na uwajibikaji katika sekta ya biashara na kwamba hiyo itasaidia kuondoa tabia zisizofaa katika biashara, na kukuza mazingira bora ya kufanya biashara, ambapo kila mtu atakuwa na nafasi sawa