Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Mkutano wa wakuu wa taasisi za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Mapinduzi Zanzibar


Naibu Waziri wa wizara ya viwanda na biashara Mhe.Exaud Kigahe ametoa rai kwa wakuu wa taasisi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha wanasimamia na kuendeleza majukumu ya Taasisi zao.

Amebainisha hayo alipokuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano wa wakuu wa taasisi za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Mapinduzi Zanzibar Januari 13,2024 katika viwanja vya maonesho ya biashara Fumba, Zanzibar.

Mhe.Kigahe amesema kuwa kutosimamiwa na kutotekelezwa kwa majukumu ya taasisi kutaathiri maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kwani utekelezaji huo unagusa pande zote mbili za Muungano.

Aidha Mhe.Kigahe ametoa wito kwa viongozi, wakuu wa Taasisi na wadau wote, kufanya kazi kwa bidii, kuwa na mashirikiano, na kufanya kazi kwa uadilifu na kwa weledi katika kutekeleza majukumu yao ili kutimiza adhma za Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania na Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Dkt.Hussein Mwinyi katika kuleta maendeleo.

Vile vile Mhe.Kigahe amepongeza kamati tendaji ya maandalizi ya mkutano huo kwa serikali zote mbili na kushauri taasisi zote za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kusajili umoja wa wakuu wa Taasisi na kuendelea kushirikiana na wakuu wa Taasisi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kukutana kila mwaka kwa lengo la kubadilishana uzoefu na fikra ambazo zitasaidia kuleta ufanisi katika utendaji.

Mkutano huo wa wakuu wa Taasisi zenye usaidizi kwa biashara na maendeleo ya viwanda umefanyika ikiwa Mataifa haya yanakaribia kutimiza miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hivyo wanahitajika kupima kiwango cha huduma na usaidizi walichowahi kutoa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kueleza mchango wao katika kutekeleza jukumu hilo sambamba na kutoa mwelekeo wa Taasisi hizo na kuonesha fursa na miradi ya maendeleo, uwezeshaji biashara na uwekezaji viwanda na mengineyo ili kuimarisha Muungano huo uwe wenye manufaa kama ambavyo waasisi walivyodhamiria