Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Mkuu wa Mkoa wa mbeya Mhe. Juma Homera ameipongeza Taasisi ya Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Mbeya


Mkuu wa Mkoa wa mbeya Mhe. Juma Homera ameipongeza Taasisi ya Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Mbeya kwa ubunifu wa kuanzisha maonyesho ya Biashara maarufu kama Mbeya MBEYA CITY EXPO.

Pongezi hizo amezitoa Mei 24 , 2024 wakati akimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe Dkt. Ashatu Kijaji ( Mb) katika ufunguzi wa maonesho hayo yanayofanyika kwa mara ya pili mfululizo katika viwanja vya Uhindini jijini Mbeya.

Maonesho hayo yenye kaulimbiu isemayo “Tuchochoee Uwekezaji na Biashara kwa Uchumi Endelevu” yatadumu kwa siku 8 kuanzia tarehe 23 Mei 2024 hadi 30 Mei 2024.

Mhe.Homera,amesema kuwa TCCIA ndiyo taasisi yenye mamlaka inayosaidia kutoa vyeti halali (Certificate of Original ambayo vimekuwa vikiwasaidia wafanyabiashara hapa nchini kutambulika nje na ndani ya nchi.

“Huu ni ubunifu mkubwa sana ambapo mmeanza kuonesha kwa kuanzisha haya maonesho na kushirikiana wadau mbalimbali wa Serikali na sekta binafsi,mmeweza kuwaalika pia mabalozi wa nchi jirani waje kujionea maonesho haya siku nyingine wasije peke yao waje na wafanyabiashara wao waone kazi inayofanyika kupitia maonesho haya”Amesema Mhe.Homera

Kwa upande wake rais wa TCCIA, Vincent Minja amesema kuwa kunafursa za kusafiri nje ya nchi wakati Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt . Samia Suluhu Hassan anapokwenda katika fursa za kibiashara kuwataka wadau hao kutumia fursa hiyo kutumia TCCIA kutambulika kimataifa Kwa kuwa na cheti halisi.

Naye Mkurugenzi msaidizi wa Maendeleo ya Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Bi.Cresencia Mwimbwa ametoa wito kwa wadau wanaoshiriki maonesho ya hayo kujifunza juu ya biashara zinazopatikana katika maonesho na kuzitumia vyema fursa adhimu za tukio hilo.