Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Mradi wa uchimbaji chuma Liganga kuanza hivi karibuni.


MRADI WA UCHIMBAJI CHUMA LIGANGA KUANZA HIVI KARIBUNI.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Suleiman Jafo (Mb) amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za kimkataba katika utekelezaji wa Mradi wa uchimbaji chuma wa Liganga ili uweze kuanza kazi mapema mwaka 2025.

Waziri Jafo ameyasema hayo Februari 18, 2025 mara alipofika katika Mradi wa Kielelezo wa Chuma wa Liganga pamoja na Mlima mdogo wa Maganga Matitu wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani Ludewa Mkoani Njombe iliyoanza Februari 17 - 19, 2025.

“Imani yetu ni kwamba ndani ya mwaka huu 2025, Mungu akijalia Mradi huu ambao ni mkombozi katika uchumi wetu kwa kuokoa fedha nyingi inayotumika kiagiza chuma nje ya nchi uanze , kwa sababu malighafi ya chuma ni muhimu sana katika ujenzi wa madaraja, barabara, majengo pamoja na matumizi mbalimbali “ Amesema Dkt. Jafo.

Akiongea na Wananchi wa Kijiji cha Mudindi Waziri Jafo amewahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuweka miundombinu wezeshi kama Barabara , umeme wa viwandani maji na huduma nyingine za kijamii ili kuuwezesha Mradi huo wa Kielelezo kutekelezeka kwa ufanisi kwa manufaa ya Taifa.

Aidha, ametoa rai kwa Wananchi wa Wilaya ya Ludewa kuchangamkia fursa mbalimbali za kibiashara kama kujenga hotel za kisasa na fursa nyingine za kibiashara mara Mradi huo utakapoanza kutekelezwa , kutunza miundombinu ya mradi huo pamoja na kishirikiana na Seeikali kihakikisha Mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) linalosimamia miradi hiyo, Bi Esther Mwaigomole amesema kuanza kwa mradi huo ambapo Liganga utadumu kwa miaka 50 na Maganga Matitu miaka 25, Tanzania rasmi itakuwa nchi ya nne barani Afrika kwa uzalishaji wa chuma.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Mhe. Olivanus Thomas amesema kuwa utekelezaji wa Mradi huo utasaidia Halmashauri kukuza mapato, kuongeza ajira na kukuza maendeleo ya Wananchi.