Habari
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Exaud Kigahe (Mb) ametoa wito kwa wahitimu kutumia elimu wanayoipata Vyuoni kuwa wabunifu,waadilifu

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Exaud Kigahe (Mb) ametoa wito kwa wahitimu kutumia elimu wanayoipata Vyuoni kuwa wabunifu,waadilifu, wenye weledi , maarifa na kujenga uchumi wa kati kupitia maendeleo ya viwanda, ili kuifanya nchi kuwa ya uchumi wa Kati wa Juu kufikia mwaka 2025.
Kigahe ametoa wito huo leo Novemba 17,2023 wakati akihutubia kwenye mahafali ya 37 na kuwatunuku wahitimu 792 wa fani mbalimbali katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Kampasi ya Dodoma.
" Wananchi wa Tanzania wamewekeza sana kwenye elimu yenu na sasa Serikali imeanza kutoa mikopo ya wanafunzi wa Vyuo vya Kati, hivyo onyesheni kuweni na heshima kwa kufanya kazi zenu kwa juhudi, maarifa na uadilifu na umakini mkubwa ili nchi yetu isonge mbele" amesema Mheshimiwa Kigahe
Aidha amesema Katika kuimarisha utoaji wa elimu na mafunzo bora, Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara itaendelea kushirikiana na CBE kwa kuboresha miundo mbinu, na kusomesha Wahadhiri wengi zaidi wa shahada za uzamili na uzamivu ndani na nje ya nchi kila inapowezekana.
Aidha, amefafanua kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha ili kuwezesha Chuo kupata miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (Public Private Partnership) ili kusaidia kupatikana kwa Fedha ili kuongeza kasi ya ujenzi wsda maktaba, kumbi za mihadhara, vyumba vya madarasa, na hosteli za wanachuo.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Prof. Edda Lwoga amesema kuwa CBE yenye walimu 103 kampasi ya Dodoma tangu kuanzishwa kwake kumekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kutoa wanafunzi bora ambao wamechukua nafasi mbalimbali Serikalini.
"Tumekuwa na makongamano ya mara kwa mara ya biashara na namna ya kujiinua kiuchumi na pia katika mwaka wa fedha 2022/23 tumeboresha miundombinu ikiwemo kujenga uzio wa chuo kizima, kumalizika jengo la maabara kupitia fedha za ndani"amesema Prof Lwoga.