Habari
Nchi ya Tanzania yang'ara katika maonesho ya Kitamaduni nchini China.
Wanafunzi wa Tanzania wanaosomea Jiangxi, wameshiriki Maonesho ya Kitamaduni ya Kimataifa ya International Cultural Festival (ICF) yaliyofanyika tarehe tarehe 14 Novemba, 2020 nchini China. Maonesho hayo ambayo hufanyika mara moja kwa mwaka yalifadhiliwa na Chuo Kikuu cha Jiangxi cha masuala ya Fedha na Uchumi (JUFE) ambapo yaliwakutanisha wanafunzi wanaoziwakilisha nchi zao, wafanyabiashara na raia mbalimbali wa nchini China. Katika maonesho hayo wanafunzi wa Tanzania waliweza kuonesha fursa za uwekezaji na biashara katika bidhaa za Korosho, Utalii, mapishi ya chakula cha asili cha Tanzania na madini ya Tanzanite ambapo banda la Tanzania lilikuwa ni miongoni mwa vivutio kutokana na maandalizi yake ambapo lilihusisha utalii wa Tanzania kwa kuonesha picha za video na vipeperushi vilivyotolewa na ubalozi wa Tanzania nchini China. Katika maonesho hayo kundi la wanafunzi wanaosomea Uzamili kutoka Tanzania ambao pia ni watumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiongozwa na afisa biashara kutoka wizara ya Viwanda na Biashara ndugu, David Geofrey walishiriki kuandaa banda la Tanzania.