Habari
KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA NA TAASISI ZAKE KWA UTENDAJI
📌 NDC, CAMARTEC na TEMDO wawasilisha taarifa za tathmini ya utekelezaji.
📌 Juhudi zinazofanywa na Wizara pamoja na Taasisi zake zimeanza kuonyesha matokeo chanya katika kuimarisha mazingira ya biashara, uzalishaji na uwekezaji nchini.
Dodoma.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na taasisi zake, ikiwemo Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Kituo cha Zana za Teknolojia Vijijini (CAMARTEC), Taasisi ya Uandisi na Usanifu wa Mitambo Tanzania (TEMDO),Tume ya Ushindani (FCC) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kwa hatua zinazochukuliwa katika kutekeleza majukumu yao na kuboresha mazingira ya kukuza viwanda na biashara nchini.
Pongezi hizo zimetolewa Oktoba 13, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Deodatus Mwanyika (Mb), wakati wa kikao cha kupokea na kutathmini taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia taasisi zake, kilichofanyika Bungeni jijini Dodoma.
Kamati hiyo imepokea mawasilisho kutoka taasisi tatu za Wizara ya Viwanda na Biashara ambazo ni NDC, CAMARTEC na TEMDO.
Taasisi ya NDC imepongezwa kwa kuendelea kutengeneza fursa za ajira kwa wananchi baada ya kuendeleza miradi ya kimkakati ya Liganga na Mchuchuma, Maganga Matitu, Kiwanda cha Kilimanjaro Mashine Tools (KMTC), pamoja na Mradi wa Magadi Soda uliopo mkoani Arusha.
Miradi hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia NDC katika kukuza sekta ya viwanda, kuongeza thamani ya rasilimali za nchi, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha fursa za ajira kwa Watanzania.
Taasisi ya CAMARTEC imepongezwa kwa kutengeneza mashine za kuwasaidia wananchi kutengeneza kuni mbadala kutokana na mabaki ya maganda ya karanga na mafunzo mbalimbali wanayoyatoa kwa wananchi ikiwemo uendeshaji wa trekta.
Kwa upande wa Taasisi ya TEMDO, imeendelea kubuni na kutengeneza mashine za kisasa zinazosaidia kuongeza thamani ya mazao ya kilimo ili kuwawezesha wananchi kuongeza thamani ya mazao yao na kuboresha maisha yao kwa ujumla.
Mhe. Mwanyika amesema juhudi zinazofanywa na Wizara pamoja na Taasisi zake zimeanza kuonyesha matokeo chanya, hususan katika kuimarisha mazingira ya biashara, uzalishaji na uwekezaji nchini.
Aidha, Mhe. Mwanyika ameitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kuendelea kuziwezesha taasisi zake katika nyanja zote ili ziendelee kutekeleza majukumu yake kwa weledi ili kuinua uchumi wa viwanda na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Denis Londo (Mb), amesema Wizara imepokea pongezi hizo pamoja na maelekezo na ushauri uliotolewa na Kamati na kuahidi kuyafanyia kazi kwa lengo la kuendelea kuinua viwanda vidogo na vikubwa, kuboresha huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi katika sekta ya viwanda na biashara.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Balozi Waziri Salum, amesema wizara inaendelea kushirikiana na taasisi zake ili kukamilisha miradi ya kimkakati na inaendelea kupokea mapendekezo mbalimbali kutoka kwa wananchi na kuyafanyia kazi ili kukuza sekta ya viwanda na biashara.
