Habari
KATIBU MKUU WA VIWANDA NA BIASHARA AKABIDHI NYARAKA ZA OFISI KWA MWENYEKITI WA BODI MPYA YA TANTRADE

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Tanzania Dkt. Hashil T. Abdallah amekabidhi nyaraka za ofisi kwa Mwenyekiti wa Bodi mpya ya wakurugenzi ya TANTRADE, Profesa Ulingeta O.L Mbamba leo katika ofisi za TANTRADE jijini Dar es salaam.
Akikabidhi Nyaraka Agosti 27, 2025 Dkt. Hashil ameiomba bodi hiyo kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha miradi mbalimbali ya Taasisi inafanya vizuri hususan Mradi wa Uendelezaji wa Uwanja wa Maonesho wa Mwl. J.K Nyerere pamoja na kuhakikisha shughuli zote za kibiashara zinazokuwa chini ya Mamlaka zinakwenda vizuri kama inavyotakiwa.
Kadhalika alisisitiza, "Bodi na majukumu yake yapo kwa mujibu wa sheria , hivyo wasimamie hayo". Vilevile, alimsisitiza Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE Dkt. Latifa M. Khamis pamoja na Menejimenti yake, kusimamia na kutekeleza majukumu ya Taasisi kwa mujibu wa Sheria.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Mbamba amesema kuwa watafanya kazi kwa ufanisi na kuhakikisha TANTRADE inaendelea mbele na kukuza biashara katika soko la dunia.