Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SEKTA BINAFSI YATAKIWA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUTATUA CHANGAMOTO


Serikali imesema itaongeza juhudi za kuimarisha sekta ya viwanda na biashara kwa kushirikiana na sekta binafsi katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili hususan umeme usiotabirika, mapungufu ya miundombinu na vikwazo vya usafirishaji na biashara.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb) Desemba 4, 2025 alipokuwa akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa 32 wa Mwaka (AGM) wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI)
uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Aidha, Waziri Kapinga ametoa wito kwa Wawekezaji na Wazalishaji kuzalisha bidhaa zenye ubora kwa bei shindani, kupanua masoko ya ndani na ya kimataifa kwa ajili ya bidhaa za Tanzania, na kuajiri vijana wa Kitanzania

Waziri Kapinga amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imechukua hatua mbalimbali katika kuimarisha msingi wa ukuaji wa viwanda endelevu kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa ya (SGR), Mradi wa Umeme wa Maji wa Mwalimu Nyerere (JNHPP), wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2115

Aidha, Waziri Kapinga pia amesema Serikali imeendelea kuongeza ufanisi wa ushughulikiaji mizigo bandarini, kukamilisha ujenzi wa uwanja mpya wa ndege wa kisasa jijini Dar es Salaam na viwanja vya kikanda kama KIA pamoja na kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI) ambao umesaidia kupunguza gharama za kufanya biashara na kuongeza tija.

Waziri Kapinga alisisitiza umuhimu wa Sekta ya Viwanda katika ukuaji wa uchumi wa taifa na alielezea mageuzi na kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwezesha wawekezaji

Naye, Mwenyekiti wa CTI, Bw. Hussein Suphian, amesisitiza kuwa ni muhimu kwa nchi kuimarisha mifumo yake ya usafirishaji ili kuendelea kuwa shindani, hasa wakati njia mpya za usafiri za kikanda zinaibuka kama Korridori ya Lobito Kati ya Angola na Zambia na Kongo DRC.

Alisisitiza haja ya kuhakikisha mifumo ya usafiri na nishati ya Tanzania inaendelea kuwa bora ili kulinda maslahi ya biashara ya nchi, kuongeza tija na kupunguza za uendeshaji