Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Bidhaa zitakazozalishwa katika Kiwanda cha LESSO hazipaswi kuuzwa moja kwa moja kwa rejareja nchini China


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb), amesisitiza kuwa bidhaa zitakazozalishwa katika Kiwanda cha LESSO hazipaswi kuuzwa moja kwa moja kwa rejareja nchini China badala yake kutafuta mawakala wa ndani ili kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata fursa za ajira pamoja kunufaika na ushirikiano huo wa kiuchumi ili kuongeza thamani katika uwekezaji na kuimarisha mnyororo wa biashara nchini.

Dkt. Jafo ametoa kauli hiyo Machi 21, 2025 wakati wa Uzinduzi wa Kiwanda hicho kipya kinachozalisha vifaa vya usambazaji maji majumbani na viwandani kinamilikiwa na wawekezaji kutoka China kilichopo Afrikana, jijini Dar es Salaam.

Dkt. Jafo Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuweka mazingira salama kwa wawekezaji kama sehemu ya jitihada za kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.

Aidha ameeleza kuwa uzinduzi wa kiwanda hicho ni moja ya mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini China, ambayo imeleta fursa mpya za uwekezaji na maendeleo.

Vilevile Dkt. Jafo amepongeza juhudi za Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso (Mb), pamoja na Ubalozi wa China nchini Tanzania kwa mchango wao katika kufanikisha uwekezaji huo. Ameeleza matumaini yake kuwa shughuli za kiwanda hicho zitaendelea kwa manufaa ya Tanzania.

Kwa upande wake Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso (Mb) amewaambia wawekezaji hao wahakikishe bei za vifaa hivyo ziwe rafiki kwa Watanzania pamoja na kupatikana kwa wakati wanapopewa kusambaza kwenye miradi.