Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

PROF. MKUMBO : TUTUMIE VIFAA VINAVYOZALISHWA NA VIWANDA VYA NDANI KWENYE UJENZI WA MIRADI HAPA NCHINI


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo ametoa wito kwa taasisi na makampuni yanayosimamia ujenzi wa miradi mbalimbali ya Serikali na binafsi kutumia vifaa vinavyozalishwa na viwanda vya ndani na kuondokana na dhana ya kuwa na hofu na kudharau bidhaa zinazozalishwa na hapa nchini.

 

Waziri Prof. Mkumbo ameyasema hayo Mei 26, 2021 Mkuranga Mkoani Pwani alipotembelea kiwanda vya Lodhia Steel Industries Ltd kinachozalisha bidhaa za chuma kama nondo na mabomba ya chuma na kiwanda cha Lodhia Plastic Industries Ltd kinachozalisha bidhaa za plastiki kama mabomba ya maji PVC na matangi ya maji ya uzajo tofauti.

 

“tunawashukuru wanaoendelea kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi hapa Tanzania ambao wanatumia vifaa vinavyozalishwa hapa ndani katika ujenzi wao lakini tunatambua pia kuna taasisi ambazo bado zina kasumba ya kutumia vifaa vya nje huku wakiamini kwamba viwanda vyetu vinazalisha vifaa vyenye ubora ambao sio sahihi lakini ukweli ni kwamba vifaa hivyo vina ubora ule ule sawa na vifaa vinavyotoka nje maana tuna taasisi zinazokagua ubora kama TBS” ameeleza Prof. Kitila Mkumbo

 

Aidha, Waziri Prof. Mkumbo amezitaka taasisi za umma na sekta binafsi zinazodaiwa na kiwanda hicho baada ya kuwauzia vifaa na kushindwa kulipa kwa muda, kulipa madeni yao ili viwanda hivyo viendelee kufanya kazi na visisimame kwasababu kiwanda kimeajiri zaidi ya wafanyakazi 1000 na wana nafasi ya kuajiri zaidi.

 

“Kuna baadhi ya taasisi za umma na sekta binafsi ambazo wameweza kuwauzia vifaa na hawajalipwa na sisi kama Wizara inayohusika na kuwezesha biashara hilo ni eneo la muhumu tunalopaswa kulifanyia kazi, tutashirikiana nao kuwakumbusha wenzetu wa taasisi hasa za Serikali ambao hawajalipa ili waweze kulipa na viwanda hivi viendelee kufanya kazi na visisimame” ameeleza Prof. Kitila Mkumbo

 

Waziri Prof. Mkumbo wakati akijibu na kutatua changamoto kubwa ya kiwanda hicho ya upungufu wa malighafi ya vyuma chakavu ameeleza kuwa Wizara itashirikisha na uongozi wa kiwanda kufanya uchambuzi wa kiwango gani cha malighfi wanahitaji pia na kiwango gani kinapatikana hapa nchini ili kujua pengo na kuweza kuongea na Wizara inayohusika na mazingira ili kujipatia kibali cha kuagiza vyuma chakavu kutoka nje.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Lodhia Group, Bw. Sailesh Pandi ameipongeza Serikali kwa kuwatembelea ili kujionea utendaji kazi wa kiwanda hicho lakini pia kusikiliza changamoto zao huku akieleza matumaini yake makubwa juu ya utatuzi wa changamoto walizozieleza kama upungufu wa malighafi ya vyuma chakavu na madeni wanayodai kulipwa na hivyo amehaidi kuendelea kuzalisha bidhaa zenye ubora.