Habari
PROF. MKUMBO: WAWEKEZAJI NA WAFANYABIASHARA WENYE NIA KUTOKA UTURUKI NA NCHI NYINGINE WAJE KUWEKEZA TANZANIA
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) ametoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji wenye nia kutoka Uturuki na nchi nyingine kuja kuwekeza na kufanya biashara kwa ubia na Tanzania na Afrika kwa ujumla ili kupata uwiano wa maendeleo (win win Situation) kwa pande zote mbili kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (African Continental Free Trade Area-AfCFTA).
Prof. Mkumbo aliyasema hayo alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu Mkataba wa AfCFTA na fursa za masoko katika Kongamano la tatu (3) la Uchumi na Biashara kati ya Uturuki na Afrika linalofanyika Istanbul Uturuki Oktoba 21 - 22, 2021. Kongamano hilo linalolenga kuimarisha uhusiano kati ya Uturuki na Afrika katika kuendeleza bishara, uwekezaji na uchumi.
Waziri Mkumbo ameambatana na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Zanzibar Bw. Omar Shaaban pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Mazingira Mhe. David Makiposa, Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Uturuki Bw. Hassani Mwamweta na wafanyabiashara wa Tanzania kuhudhuria Kongamano hilo nchini Uturuki.
Akiwasilisha mada yake Prof. Mkumbo amewasihi wawekezaji kutoka Uturuki kuja kuwekeza Tanzania na Afrika kwa ujumla kwa kuwa Mkataba AFCFTA unawezesha upatikanaji wa soko la bidhaa na huduma lenye idadi ya watu takriban bilioni 1.2 ambapo hadi sasa nchi 44 za Afrika zimeridhia Mkataba huo ulioanza kutekelezwa tangu Mei 30, 2020.
Amesema mpaka sasa Mataifa ya Afrika yamepata uhuru wa Kisiasa sasa yaongeze nguvu katika kujikomboa kiuchumi ili kufikia malengo ya Agenda 2063 ya Afrika yenye lengo la kuhakikisha kuwa Afrika inakomesha maisha ya bunduki ndani ya Afrika, kukuza Uchumi, kutunza Amani, kuendeleza Elimu na Sekta ya Viwanda na teknolojia kwa kutumia mkataba wa AfCFTA.
“ Muda wa kuomba msaada kutoka nchi zilizoendelea umepita, na amewasihi wawekezaji wenye nia waje wawekeze Tanzania yenye maliasili na malighafi za kutosha na vijana wengi wenye nguvu na elimu”. Amesema Prof. Mkumbo.
Prof. Mkumbo amewakaribisha wawekezaji wenye nia kutoka Uturuki na nchi nyingine kuja kuwekeza Tanzania katika maeneo ya uchakataji mazao, afya, nishati, madini, utalii. Na tunawakaribisha kutembelea Mlima Kilimanjaro ambao ni Mlima wa pili kwa urefu Afrika, fukwe za Zanzibar, na mbuga za wanyama.
Naye Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Zanzibar Bw. Omar Shaaban alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu fursa za uwekezaji katika Kongamano hilo, aliwakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania na Zanzibar yenye idadi ya watu takriban milioni 60 ambayo inatoa fursa nyingi za uwekezaji, mazingira bora ya kufanya Biashara, maliasili, vivutio vya utalii, malighafi za kutosha, Uchumi wa bahari na soko la uhakika la bidhaa.
Wakati huohuo, Waziri Mkumbo na Ujumbe wake wamefanya mazungumzo na kukubaliana na Waziri wa Biashara wa Uturuki Mhe. Dkt. Mehmet Mus kuhusu kuimarisha na kuendeleza ushirikiano baina ya Tanzania na Uturuki katika kuendeleza na kukuza biashara baina ya nchi hizo mbili.
Aidha, Waziri Mkumbo pamoja na ujumbe wake pia wamefanya mazungumzo kuhusu uendelezaji wa kilimo cha chai, kutafuta masoko na kuhaulisha teknolojia mpya ya kilimo hicho na Mmiliki wa Kampuni ya Beta Food Industry and Trade Inc Mehmet Ali Ugur ambaye amekubali kuja Tanzania kuwekeza katika ujenzi wa kiwanda cha kusindika chai pamoja na kununua chai inayolimwa Tanzania.
Vilevile Waziri na Ujumbe wake pia walifanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya Usindikaji wa Mazao ya Kilimo, Botek Bosphorus Techinical Consulting Corp ambaye ameonesha nia ya kuja Tanzania kuwekeza katika usindikaji wa mazao ya vyakula, matunda na mboga mboga na kuyauza nje ya nchi.
Pamoja na hayo, Waziri Mkumbo na ujumbe wake pia wamefanya mazungumzo kuhusu kuendeleza sekta ya uzalishaji dawa nchini na kupunguza uagizaji wa dawa nje ya nchi na wamiliki wa viwanda vya uzalishaji dawa za binadamu wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya DINCSA Pharma Bw. Aytac Dincer ambaye ana mipango ya kuanzisha kiwanda cha kutengeneza dawa, vifaa tiba na vitendanishi nchini Tanzania.
Waziri Mkumbe na ujumbe wake wmeshiriki Kongamano hilo la Biashara lililoratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Uturuki ukishirikiana na Wizara, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania, Kampuni ya Go Extra Mile Safaris na Benki ya CRDB iliyodhamini wafanyabiashara 100 kuhudhuria kongamano hilo kwa lengo la kujifunza, kubadilishana uzoefu, kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania na kuimarisha ushirikiana kati ya wafanyabiashara wa Tanzaniana Uturuki.