Habari
Prof. Shemdoe atembelea kiwanda cha Nellkanth Chemical L.t.d kilichopo eneo la Amboni jijini Tanga.
KATIBU Mkuu wizara ya viwanda na biashara Prof. Riziki Shemdoe ametoa wito kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini waje katika mkoa wa Tanga kwani yapo maeneo mengi ya kuwekeza katika sekta viwanda. Wito huo aliutoa jana alipotembelea kiwanda cha Nellkanth Chemical L.t.d kilichopo eneo la Amboni jijini Tanga wakati alipofanya ziara ya siku moja. Prof. Shemdoe alisema kuwa Tanzania inavutia zaidi katika uwekezaji na maeneo mengi ya uwekezaji yapo na yanatekelezwa kwa ajili yao hivyo kuwataka wawekezaji wanaohitaji waje kuwekeza ili walipe kodi, walete ajira na mambo mengine yanayoendana na uwekezaji. “Wito wangu kwa wawekezaji wengine waje wawekeze Tanzania, waje wawekeze mkoa wa Tanga kuna maeneo mengi sana na magodauni ambayo yapo kwa sasa na yangeweza kutumika kwa ajili ya viwanda, waje wakijua hapa nchini tuna blue print ambayo inatekelezwa kwa ajili ya wawekezaji ili waje walipe kodi na kuleta ajira kwa wananchi wetu” alisema. Aidha alizungumzia suala la uzalishaji katika kiwanda hicho na kusema kuwa kiwanda hicho kina maeneo makubwa yanayofaa kuwekeza biashara zaidi ya uzalishaji uliopo wa chokaa kwani wana maeneo mengine zaidi ya ekari 2,500 ambayo wanaweza kulima chumvi ambayo imeshaanza kuonekana. “Eneo hili zamani lilikuwa halilimiki hapa lakini sasa kuna migodi ambayo inatoa madini ambayo inazalishwa na kuleta faida nchini kwani wanalipakodi na kusaidia wananchi kupata ajira, vilevile kuanzishwa kwa shamba hili kutatufanya sisi kuacha kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi” alibainisha. Hata hivyo alisema kuwa kiwanda hicho kimefanya kazi kubwa kutokana na uzalishaji wake kwani wameajiri wananchi zaidi ya 2,000 ambao wako kiwandani hapo na wengine takribani 4,000 wako kwenye maeneo mengine ambayo yanamilikiwa na mwekezaji huyo. Naye Mkurugenzi mzalendo wa kiwanda hicho Rashid Amour (Liemba) alisema kuwa kupitia uzalishaji mkubwa wa kiwanda hicho tayari wameshateka masoko katika nchi mbalimbali za Afrika mashariki na Maziwa makuu ambapo wamekuwa wakipeleka bidhaa zao katika masoko ya ushindani. “Kwakweli mpaka sasa hivi soko letu kubwa liko Congo, lakini siyo Congo pekeyake bali tumeziteka nchi za Kenya, Burundi, Rwanda na Uganda, kwa sasa hivi bidhaa yetu tunashukuru tumezishika nchi zote za Afrika mashariki maana wao ndiyo wanapambana na sisi” alifafanua Liemba. “Kama mnavyofahamu biashara ni ushindani na sisi tumeingia kwenye ushindani na nchi hizi, tunaiomba serikali iweze kutusaidia katika ushindani huu na kama itatusaidia nina hakika ushindani huu tutaushinda bila matatizo” aliongeza. Aidha alieleza kwamba kwa sasa ushindani mkubwa wanaoupata ni kutoka nchi ya Afrika kusini ambako pia alizungumzia hofu yake kuhusu soko hilo kwamba nchi ya Congo imeshaingiliwa na nchi ya China ambayo inatengeneza bidhaa hiyo ya chokaa kupeleka huko. “Kwa sasa hivi ushindani wetu mkubwa uko South Africa kwa Congo, sasa hivi Congo wameingia wachina, wachina wanajitahidi sana kutengeneza bidhaa kuleta hapa nao ni chokaa kama sisi na mpaka sasa hivi tunajitahidi kupambana nao” aliongeza. Hata hivyo alibainisha kwamba kiwanda hicho kinapambana katika soko la chokaa lakini zipo biashara nyingine wanazozalisha kama vile magnissium (MGO) ambavyo vyote vinatumika kusafishia cooper ambapo pia alitoa takwimu ya bidhaa wanazosafirisha kupeleka kwenye masoko nje ya nchi. “Congo peke yake tunapeleka siyo chini ya tani elfu kumi lakini kipindi cha nyumba tulikuwa tunakwenda mpaka tani elfu ishirini, Kenya na Zambia nako pia tunapeleka tani kumi vilevile kwahiyo ni tani elfu ishirini kwa mwezi” alifafanua.