Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Rais Dkt. Magufuli azindua kiwanda cha Vigae


Rais Dkt. Magufuli azindua kiwanda cha Vigae Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt John Pombe Magufuli mapema ameweka jiwe la msingi katika kiwanda cha kutengeneza vigae (Tiles) cha Goodwill Tanzania Ceramic Limited kilichopo kijiji cha Mkiu Wilaya ya Mkuranga, Pwani. Ujenzi wa kiwanda cha Goodwill Ceramic Tanzania Limited umegharimu Dola za kimarekani Milioni 50, awamu ya kwanza na ina uwezo wa kuzalisha mita mraba 80,000 za vigae kwa siku, kitatoa ajira za moja kwa moja 1,000 na ajira zisizo za moja kwa moja 2,000.Kiwanda hicho kitatumia asilimia 95% ya malighafi kutoka Tanzania na asilimia 5% ya malighafi itatoka nchini China.   Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi la kiwanda hicho Mhe. Magufuli alisema amefurahishwa na ujenzi wa kiwanda hicho kikubwa Afrika Mashariki na ameishukuru menejimenti ya kiwanda hicho kwa kuwekeza Tanzania. “Nchi hii tumechezewa vya kutosha, sasa nyinyi hapa mnayeyusha mchanga kwa kuuchemsha hadi nyuzi joto 1,000 wakati wengine wanasafirisha mchanga nje ya nchi wakati uchemshaji wake hauhitaji kufika nyuzi joto 1000, naangiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Wizara ya Nishati na Madini kuwa kuanzia sasa ni marufuku kusafirisha mchanga nje ya nchi,” alisisitiza Mhe. Rais Magufuli. Aidha Rais Magufuli aliwapongeza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Watendaji wa Mkoa wa Pwani na Serikali ya China kwa kuwavutia wawekezaji kuwekeza katika mkoa wa Pwani. “Nilihaidi katika kampeni yangu kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, Hakuna nchi inayoweza kuendelea bila kuwa na viwanda. Viwanda ni kipimo kimoja wapo cha maendeleo.” Mhe.Magufuli aliwahakikishia wawekezaji hao usalama wao na mali zao katika Mkoa wa Pwani na Tanzania kwa ujumla. “Msiwe na wasiwasi serikali imejipanga kupambana na wahalifu katika mkoa wa Pwani, nawaalika na wawekezaji wengine kuja kuwekeza kwa kuwa mkoa huu ni kati ya mikoa yenye viwanda vingi. Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dkt.Adelhelm Meru alisema tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani jumla ya viwanda 2,169, vinavyojumuisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vimesajiliwa na kituo cha uwekezaji TIC na vipo katika hatua mbalimbali za uendelezwaji. Naye Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Dkt Lu Youging alimpongeza Mhe.Magufuli kwa kutilia mkazo na kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi unaokuwa kwa kasi na Serikali ya China itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kujenga viwanda.