Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DKT. SAMIA SULUHU HASSAN ATAKA MIKAKATI ENDELEVU YA KUWAWEZESHA WANAWAKE KIBIASHARA


MHESHIMIWA Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka washiriki wa Kongamano la Pili la Wanawake katika Biashara ndani ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA)kujadili namna ya kuwezesha ushiriki imara wa wanawake katika biashara ndani ya bara la Afrika.
 
“Ni muhimu sana katika Kongamano hili mkaja na mipango mahsusi ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa na kuimarisha ushirikiano kwa lengo la kuwa na ushiriki wenye tija kwa wanawake katika biashara unakamilishwa”
 
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo (Jumatano, Desemba 6, 2023) alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia  katika ufunguzi wa Kongamano hilo linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. 
 
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kufanyika kwa Kongamano hili kwa mara ya pili ni ishara tosha ya kuonyesha dhamira ya Nchi Washiriki wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika kukuza ushiriki wa wanawake katika biashara chini ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika.
 
“Kufanyika kwa Makongamano haya kunatoa nafasi muhimu kwa wadau mbalimbali wa kuwawezesha wanawake kujadiliana na kutafuta ufumbuzi wa pamoja wa changamoto zinazokwamisha jitihada za wanawake katika biashara”
 
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa miongoni mwa faida za kuwa na Eneo Huru la Biashara la Barani Afrika ni kusaidia kuongezeka kwa biashara baina ya nchi za Afrika kutokana na nchi kuondoleana ushuru wa forodha “Faida Nyingine ni kushughulikia kwa pamoja vikwazo vya biashara visivyo vya kodi na kukuza uongezaji thamani wa malighafi zinazozalishwa ndani ya Afrika”
 
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imeanzisha Mfumo Rahisi wa Biashara (Simplified Trade Regime – STR) kwa ajili ya mauzo ya nje ya mipakani kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara wadogo wa mipakani.