Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mgeni rasmi katika maonesho ya 45 ya sabasaba mwaka 2021.

ais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ambayo yanafanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere maarufu kama Sabasaba yaliyoanza Juni 28 na kutarajiwa kumalizika Julai 13, mwaka huu
Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kukagua maandalizi ya maonesho yatakayozinduliwa rasmi tarehe 5 Julai, 2021.
Prof. Mkumbo amezungumza na waandishi wa habari kuhusiana na jinsi Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ilivyojipanga kuhakikisha maonesho haya ya mwaka huu yenye kauli mbiu ya “Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu” yanakuwa mazuri na ya mfano.
Prof. Mkumbo amesema kuwa mwaka huu kutakuwa na washiriki 3,002, taasisi za umma na binafsi zitashiriki na pia kumekuwa na ongezeko la nchi zitakazoshiriki mwaka huu kutoka nchi tano hadi nchi saba ambapo makampuni ya kigeni ni sabini na sita 76.
Mhe. Prof. Mkumbo ameeleza kuwa mwaka huu kutakuwa na mikutano ya mitandao ya B2B itakayowakutanisha wafanyabiashara wa nje na wa kwetu katika kutafuta fursa za uwekezaji.
Pia kutakuwa na nembo maalumu ya banda maalumu ya viungo vya vyakula vinavyozalishwa nchini na uzinduzi huo utafanyika tarehe 9 Julai, 2021, pia uzinduzi wa mfumo rasmi wa taarifa za biashara, pia kutakuwa na uzinduzi wa duka la mtandao unaoanzishwa na Tantrade kwa kushirikiana na benki ya posta, pia kutakuwa na uzinduzi wa Trailer lililotengenezwa na Kilimanjaro Machine Tools, uzinduzi wa utambuzi wa mabanda ya washiriki wa ndani ya uwanja.
Prof. Mkumbo amewataka wanachi kujitokeza kwa wingi kwani viingilio ni nafuu kwa kila Mtanzania kuja kujionea biashara mbalimbali na kupata fursa mbalimbali.
Aidha Prof. Mkumbo amesema kuwa maonesho ya mwaka huu yatazingatia muongozo uliotolewa na wizara ya afya kuhusu kujikinga na homa kali ya mapafu (COVID19).
Pia Prof. Mkumbo amewataka washiriki wote kuhakikisha wanazingatia hatua zote za kujikinga na ugonjwa huu kwa kuweka vitakasa mikono na maji tiririka ili wanachi waweze kujikinga na ugonjwa huu wa (COVID19).
"Tunasisitiza na kuhimiza wananchi wetu ambao watatembelea Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara kuvaa barakoa, tumeongea na wenzetu wa Bohari ya Dawa(MSD) kuleta barakoa ili wananchi wasiokuwa nazo waweze kununua wafikapo eneo la maonesho, pia tumeweka sehemu za kunawia mikono na vitakasa mikono katika sehemu mbalimbali.