Habari
TAFITI NA MASOKO NJE YA NCHI NGUZO YA MAENDELEO YA BIASHARA – WAZIRI KATAMBI
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Patrobas Katambi (Mb), amesema tafiti ni nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kibiashara, akisisitiza kuwa bila tafiti hakuna mafanikio ya kweli.
Amesema hayo katika ziara aliyoifanya katika Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Desemba 20,2025 Jijini Dar es Salaam.
Amesema tafiti husaidia kubaini maeneo yaliyokosewa, yale yaliyofanyika vizuri, nani alifanya nini na kwa wakati gani, hivyo kutoa msingi wa kufanya maboresho na kujifunza pamoja na kuwa dira ya maamuzi ili kujifunza kutokana na makosa ya wengine na kuepuka kuyafanya tena pamoja na kujifunza kutoka katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea ili kufanya yaliyo sahihi na kuacha makosa.
Katambi amesisitiza umuhimu wa ukusanyaji wa taarifa za masoko kama wajibu wa msingi, ndani na nje ya nchi, pamoja na kulinda na kusimamia Muungano kwa kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha, amesema TanTrade ni taasisi muhimu katika kukuza uchumi wa taifa kwa kuongeza mapato, ajira na fursa kwa wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Dkt. Latifa Khamis, amesema taasisi hiyo imefanya utafiti kwa biashara 334, hatua iliyowezesha kuboresha maeneo mbalimbali ya biashara.
Ameeleza pia kuwa TanTrade imeendesha kliniki za shughuli za biashara kwa ajili ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara pamoja na kufanikisha uanzishaji wa nembo ya “Made in Tanzania” kwa ajili ya kutambulisha na kulinda bidhaa za Tanzania.
Kwani hadi sasa, bidhaa 30 zimeshasajiliwa, na ifikapo Oktoba mwaka ujao 2026, makampuni yote yanatakiwa kuanza kutumia nembo hiyo.
