ZAO LA MWANI ,KATANI NA KOROSHO KUINGIZWA KWENYE MFUMO WA STAKABADHI GHALANI.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe Dkt. Selemani Jafo (Mb.) ameiagiza Bodi ya Stakabadhi za Ghala kuhakikisha zao la Mwani, linakuwa zao la kwanza kuingizwa kwenye Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika Mkoa wa Tanga likifuatiwa na Katani, Korosho ,kilimo cha mbogamboga na matunda.
Ameyasema hayo akiongoza Kikao cha wadau wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala Kidigitali kilicholenga kujadili namna bora ya kutumia Mfumo huo katika kunufaisha wazalishaji wa bidhaa hususan za kilimo kwa kuwapatia bei shindani iliyopo sokoni kilichofanyika Aprili 11, 2025 Mkoani Tanga.
Dkt. Jafo pia amewashauri Vongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Madiwani na Viongozi wa Serikali za Mitaa pamoja na Vyama vya Ushirika kutoa elimu na kuihamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika mfumo huo wenye manufaa makubwa kwa Wakulima na Taifa kwa ujumla.
Aidha, ametoa rai kwa Taasisi za umma na binafsi kuchangamkia fursa kwa kuwekeza katika ujenzi na uendeshaji wa maghala, usafirishaji wa mazao, na uongezaji thamani kwa bidhaa zinazohifadhiwa na kuuzwa kupitia Mfumo huo ili kuhakikisha miundombinu ya hifadhi ya mazao inapatikana mara mfumo huo utakapoanza kutekelezwa rasmi.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian amebainisha kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani utawasaidia wakulima kupata thamani halisi ya mazao yao, kuongeza tija, kipato huku ukileta mageuzi katika sekta ya kilimo na biashara kwa mkoa wake huku akiahidi kuchagua mazao kumi yatakayochukuliwa katika mfumo huo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) Ndg.Asangye Bangu, amesema kuwa kwa kushirikiana na wizara pamoja na wadau mbalimbali, taasisi hiyo ipo tayari kutoa msaada kwa wakulima wanaouhitaji kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na kupendekeza pia kuingizwa kwa zao la dagaa katika mfumo wa stakabadhi ghalani. Alisema kuwa kwa sasa wavuvi wanalazimika kuuza dagaa kwa bei ya chini kutokana na kukosa mfumo rasmi wa uhifadhi na uuzaji.