Habari
Serikali kuhakikisha viwanda vyote vya kuchambua pamba vinafanya kazi nchini

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exhaud Kigahe (Mb) amesema Mkakati wa Serikali ni kuhakikisha viwanda vyote vya kuchambua pamba vinafanya kazi nchini
Amesema hayo Novemba 6,2023 Bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Hamis Mwagao Tabasam, kuhusu lini Serikali itavikarabati Viwanda vya kuchambua Pamba vya Nyakarilo, Nyamirilo na Buyagu vilivyopo Sengerema?
Kigahe amesema Serikali kupitia Bodi ya Pamba (TCB) mwaka 2020, ilifanya Tathmini ambayo imewezesha baadhi ya viwanda vinavyomilikiwa na Vyama vya Ushirika kupata mikopo kupitia Benki ya Kilimo (TADB) iliyowezesha kukarabati viwanda vyao. Kupitia utaratibu huo, Serikali itahakikisha pia viwanda vya Nyakarilo, Nyamirilo na Buyagu vinakarabatiwa ili kuongeza tija katika mnyororo mzima wa Sekta ya Pamba.
Vile vile amesema Viwanda vya kuchambua pamba vilivyo na usajili wa Bodi ya Pamba (TCB) hadi kufikia mwishoni mwa msimu (cotton Ginning) wa 2022/2023 vilikuwa 92, kati ya hivyo viwanda 57 vinamilikiwa na Makampuni Binafsi na 35 ni mali ya Vyama vya Ushirika.
Aidha amesema Wizara ya Viwanda na biashara itashirikiana na Wizara ya Kilimo kufufua viwanda hivyo na kuweka mikakati yakuwawezesha kupata mitaji kupitia benki ya Kilimo nakuchochoea kilimo cha pamba