Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Serikali yaahidi kutatua tozo ya makontena


Serikali yaahidi kutatua tozo ya makontena.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mh. Dkt. Selemani Jafo, amewahakikishia wafanyabiashara kuwa Serikali itafanyia kazi malalamiko yao kuhusu tozo ya kupandisha na kushusha makontena.

Vikevile Waziri Jafo amesema ndani ya siku 60 Serikali itaitisha Mkutano mwingine baada ya kukaa na sekta husika ili kupata muafaka na kutoa mrejesho kwa wafanyabiashara.

Waziri Jafo amesisitiza kuwepo na mazingira bora Viwandani sababu kwa sehemu kubwa vinatoa ajira kwa vijana, na kuwawezesha kujikimu na kuongeza mafanikio katika sekta ya Viwanda.

Ameyasema hayo Februari 10,2025 katika Mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam uliowakutanisha Wanachama wa Shirikisho la Wamiliki wa Viwanda Tanzania (CTI) na Viongozi wa Serikali

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdalah amesema Wafanyabiashara wako tayari kulipa kodi na wanahitaji kujua kiasi cha kodi kwanini wanalipa na kwa namna gani.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Toba Nguvila, ameeleza kuwa viongozi wa mkoa huo hawatakuwa kikwazo katika kutafuta suluhisho la changamoto hiyo na Mkoa wake uko tayari kushirikiana na sekta husika ili kuhakikisha mazingira ya biashara yanaboreshwa.

Naye Mkurugenzi wa CTI), Bw. Leodegar Tenga, alisema kuwa ndani ya siku 60 wanatarajia kupata majibu yatakayosaidia sekta ya viwanda na uchumi kwa ujumla.

Aidha amebainisha kuwa viwanda vina mchango mkubwa kwa serikali kupitia mapato na ajira, hivyo ni muhimu kutafuta suluhisho la tozo hiyo.