Habari
Serikali yahimiza uwekezaji katika viwanda vya mbolea.

Serikali inaendelea na mkakati wa kuhimiza na kutangaza fursa za uanzishwaji wa viwanda vya mbolea ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya Mbolea nchini
Hayo yamebainishwa Bungeni Februari 09,2024 na Naibu waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde kwa niaba ya Naibu waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe wakati akijibu swali la msingi la Mbu ge wa Kilwa Kusini, Mhe.Ally Mohamed Kassinge.
Katika swali lake, Kassinge alitaka kujua mazungumzo kati ya Serikali na Mwekezaji wa Kiwanda cha Mbolea Kilwa Masoko kutokana na Gesi Asili ya Songosongo yamefikia hatua gani.
Akijibu swali hilo Mhe.Silinde amesema Serikali inaendelea na majadiliano na wawekezaji mbalimbali wakiwemo Kampuni ya HELM, FERROSTAAL na PolyServe ili kuharakisha uwekezaji wa kiwanda cha mbolea Kilwa Masoko.
Aidha Mhe.Silinde amebainisha kuwa Kwa sasa Serikali inaendelea kuhimiza na kutangaza fursa ya uanzishwaji wa viwanda vya mbolea nchini ikiwemo eneo la Kilwa Masoko kutokana na uhitaji mkubwa wa mbolea hapa nchini.