Habari
Simamieni Sheria ya Vipimo

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa ameuagiza uongozi na Watumishi wa Wakala wa Vipimo Nchini kuhakikisha wanasimamia vyema sheria ya vipimo na kanuni zake kwa kukagua na kuhakiki mara kwa mara vipimo vinavyotumika kuhakiki ili kumlinda mlaji na muuzaji ili kuweka thamani halisi ya bidhaa.
Mhe.Majaliwa ameyasema hayo Februari 06, 2024 wakati akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kuweka Jiwe la Msingi katika Jengo la Makao Makuu ya Ofisi ya Taasisi ya Wakala wa Vipimo (WMA) iliyopo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara Jijini Dodoma.
Aidha ameuelekeza Wakala huo kuweka utaratibu mahususi wa ufungashaji wa mazao ya Biashara usiozingatia vipimo sahihi maarufu kama Lumbesa NA na kuhakikisha wanaondoa malalamiko ya wakulima ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo wahanga wa kudhulumiwa kwa kulazimishwa kufungasha kwenye ujazo ambao haukubaliki kisheria.
Vilevile Mhe.Majaliwa amewataka wananchi nchini kuwa waangalifu katika ununuzi wa bidhaa kwa kuzangatia na kuwa makini katika vipimo ili kuepuka udanganyifu Pamoja na wafanyabiashara wote Nchini kuzingatia taratibu na kanuni za vipimo vilivyowekwa na Serikali na kuacha mtindo wa kuchezesha mizani bali watumie vipimo vya halisi na vya haki.
Naye Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amesema ujenzi wa jengo hilo utakaogharimu shilingi bilioni 6.17 hadi kukamilika kwake ni sehemu ya juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uboreshaji wa mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa umma na upatikanaji wa huduma mbalimbali za vipimo nchini ikiwa ni Pamoja na Maabara na vifaa vya kisasa
Kwa Upande wa Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo,Bi Stella Kahwa alisema ujenzi wa mradi huo unaojengwa kwa kipindi cha miezi 30 ulianza rasmi tarehe 01 Julai, 2022 na utakamilika tarehe 25 Januari,2025 na mpaka sasa ujenzi huo umefikia asilimia 70.36.