Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Taasisi za Umma Tumieni Tafiti za Taasisi za Elimu ya Juu


Taasisi za Umma Tumieni Tafiti za Taasisi za Elimu ya Juu

Rais Mstaafu wa Tanzania Dkt .Jakaya Mrisho Kikwete ametoa rai kwa Taasisi za Umma kuanza kutumia matokeo ya tafiti kutoka Taasisi za Elimu ya Juu kama vile Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) ili kupata matokeo chanya katika shughuli zao.

Ametoa rai hiyo Novemba 22, 2023 wakati akifungua Kongamano la nne la Maendeleo ya Biashara na Uchumi 2023 lililoandaliwa na CBE jijini Dodoma ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa.

Dkt . Kikwete pia amesema Kongamano hilo linawawezesha Watanzania, hususani vijana, kupata hamasa ya kuongeza ubunifu na kufanya shughuli za ujasiriamali wa kiteknolojia wakienda sambamba na mabadiliko ya kiuchumi Duniani.

Amesema licha ya umuhimu wa Makongamano haya, bado kumekuwa na msukumo mdogo wa kusambaza na kutumia matokeo ya tafiti hizo kwa upande wa Serikali, wadau na wananchi kwa ujumla.

"Naziomba Taasisi za Elimu ya Juu zinazofanya tafiti kutambua kuwa zina wajibu wa kuhakikisha matokeo ya tafiti wanazofanya zinawafikia walengwa hususani wananchi wa kawaida na kwa lugha rahisi inayoeleweka."Amesema Rais Mstaafu Kikwete.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dkt. Ashatu Kijajii (Mb) akizungumza kwenye Kongamano hilo amesema kuwa Kongamano hilo limebeba Kauli mbiu isemayo “Mazingira
ya Biashara na Uwekezaji kwa Maendeleo ya Kiuchumi” kwa lengo la kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini.

"Ni matumaini yetu kuwa,kupitia Mkutano huu tutasikia tafiti zinazoeleza mafanikio mbalimbali yaliyopatikana lakini pia na changamoto ambazo bado zimeonekana kuwa kikwazo katika kufikia malengo ya Serikali na kutumia tafiti hizo kuboresha zaidi. ". Amesema Dkt. Kijaji

Mwisho.