Habari
Tanzania na Uturuki Zimepanga Kuongeza Ushirikiano wa Kiuchumi Kufikia Dola Bilioni 1.
Serikali ya Tanzania na Uturuki zimedhamiria kuongeza ushirikiano wa kiuchumi kupitia biashara na uwekezaji katika sekta za kimkakati ikiwemo kilimo, miundombinu na teknolojia ili kusaidia nchi hizi mbili kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma kufikia wastani wa dola bilioni 1.
Yameelezwa hayo Julai 23, 2025 jijini Dar es salaam na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Selemani Jafo wakati akisaini Tamko la kuanzisha Kamati ya Pamoja ya Biashara kati ya nchi hizi mbili itakayokuwa na jukumu la kushughulikia majadiliano yanayohusu biashara na kuondoa vikwazo vya kibiashara kati ya nchi hizi mbili
Akizungumza Dkt. Jafo amesema Mauzo ya bidhaa kati ya nchi hizi mbili bado ni kidogo akiweka bayana kuwa Takwimu za mwaka 2024 zinaonesha Tanzania kuuza bidhaa nchini Uturuki zenye thamani ya dola milioni 284 huku uturuki ikiuza nchini bidhaa zinazokadiriwa kuwa na thamani ya dola milioni 217.
Aidha, Alisema mahusiano kati ya Tanzania na Uturuki yameimarika kwa kasi, hasa tangu kufunguliwa tena kwa Ubalozi wa Uturuki nchini Tanzania mwaka 2009 na kuanzishwa kwa Ubalozi wa Tanzania Uturuki mwaka 2017.
Kwa upande wake Kaimu Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Mhe.Ali Goktug IPEK amesema Tamko hilo ni jukwaa muhimu katika kusaidia kukuza biashara kati ya nchi hizi mbili.
Tanzania inauza bidhaa za mazao ya kilimo nchini uturuki huku uturuki ikiingiza zaidi bidhaa za nguo na mitambo inayotumika kwa ajili ya shughuli za miradi nchini.