Habari
TANZANIA YAENDELEA KUTAFUTA FURSA ZA VIWANDA KUPITIA UCHUMI WA BULUU.
📌Naibu Waziri Londo ashiriki mkutano wa COP12 kunadi fursa za viwanda;
📌wawakilishi kitoka nchi 10 za Afrika washiriki.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, ameshiriki Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), unaofanyika katika ukumbi wa JNCC jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 6 hadi 9, 2026, kwa lengo la kujadili mustakabali wa mazingira ya bahari na Uchumi wa Buluu katika Bahari ya Hindi Magharibi.
Mkutano huo unaowakutanisha wawakilishi kutoka nchi 10 wanachama unatoa fursa kwa nchi hizo kujadili namna ya kutumia rasilimali za bahari kwa njia endelevu huku zikilinda mazingira na kuongeza manufaa kwa wananchi, miongoni mwa maeneo yanayojadiliwa ni uwekezaji katika uvuvi, ufugaji wa viumbe vya majini, utalii wa baharini na kilimo cha Mwani, sekta ambazo zina nafasi ya kuchochea shughuli za uzalishaji na biashara.
Kwa Tanzania, ushiriki wa Mhe. Londo unaongeza mtazamo wa sekta ya viwanda na biashara katika mjadala wa Uchumi wa Buluu, hususan katika kutambua fursa za kuongeza thamani ya rasilimali na kukuza shughuli za kiuchumi zinazotokana na bahari, COP12 inalenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na changamoto za uchafuzi wa bahari, mabadiliko ya tabianchi na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za bahari.
Mkutano huo umefunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uhifadhi na usimamizi endelevu wa mazingira ya bahari, huku akieleza nafasi ya Uchumi wa Buluu katika kukuza shughuli za kiuchumi na kuongeza fursa kwa wananchi.
