Habari
anzania bado haijatumia kikamilifu fursa za kufanya biashara katika soko la Marekani la AGOA.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Exaud Kigahe amesema kuwa Tanzania bado haijatumia kikamilifu fursa za kufanya biashara katika soko la Marekani la AGOA.
Amebainisha hayo wakati wa mkutano wa kibiashara kati ya Tanzania na Marekani ulioangazia fursa za kibiashara zinazoweza kutumiwa na pande zote mbili Machi 11, 2025, jijini Dar es Salaam.
Mhe.Kigahe amesema ni wakati sasa wa Watanzania kuendelea kutumia fursa hiyo kutokana na ushirikiano wa Tanzania na Marekani kwani moja ya malengo ya ushirikiano huo ni kusaidia kulifiakia soko la AGOA pamoja na kuwasaidia wajasiriamali wadogo kuongeza thamani ya bidhaa zao, kutoa ajira nyingi kwa vijana, kupata masoko ya uhakika kwa bidhaa zao, na kuongeza fedha za kigeni.
Aidha katika mkutano huo wa kibiashara kati ya Tanzania na Marekani, wawekezaji kutoka Marekani wameonesha nia ya kuwekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo hasa kwenye mazao ya chai na kahawa pamoja na sekta ya madini kwa lengo la kuyaongezea thamani.
Pia amesema Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan inaendelea na jitihada za kuzalisha wajasiliamali wadogo na kuwapa elimu kupitia ushirikiano na Mataifa mbalimbali ikiwemo Marekani ili kuwafanya kuwa wafanyabiashara wakubwa pamoja na kuweka mitaala ya ujasiriamali shuleni.