Habari
Dhamira ya Serikali ya Tanzania ni kuendelea kuweka Mazingira wezeshi ya Uwekezaji na Biashara nchini
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt.Suleiman Serera amesema kuwa dhamira ya Serikali ya Tanzania ni kuendelea kuweka Mazingira wezeshi ya Uwekezaji na Biashara nchini hali ambayo inachagiza uchumi wa nchi.
Dkt.Serera amebainisha hayo wakati wa Uzinduzi wa Jubilei ya Dhahabu na Kifungashio kipya maalum cha Unga wa ngano wa Kampuni ya Azam , Juni 17,2025 Katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam.
Dkt.Serera amesema kuwa Miaka hamsini ya Jubilei ya Dhahabu hiyo na Kifungashio kipya maalum cha Unga wa Ngano ni ishara kuwa Kampuni hiyo imeweka mfano wa kuigwa katika ubunifu wa vifungashio, uendelezaji wa viwanda pamoja na uwajibikaji kwa jamii hasa kwa kutoa ajira nyingi nchini.
Aidha Dkt.Serera amewaasa Viongozi wa Kampuni hiyo ya Bakhresa kuendelea kuifanya Kampuni hiyo kuwa kampuni inayopiga hatua zaidi ndani ya miaka mingine 50 ijayo.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Said Salim Backresa Co.Ltd Bw.Ali Asgar amesema kuwa ndani ya Miaka hamsini wanajivunia kuwa na kiwanda chenye uwezo wa kusaga tani 4000 ukilinganisha na hapo awali ambapo walikuwa na uwezo wa kusaga ngano tani 15 kwa siku.