Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

TANZANIA KUSHIRIKI MAONESHO YA EXPO 2025 NCHINI JAPAN.


TANZANIA KUSHIRIKI MAONESHO YA EXPO 2025 NCHINI JAPAN.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt. Selemani Jafo(Mb) amesema Tanzania inatarajiwa kushiriki maonyesho ya Dunia ya Expo 2025 yatakayofanyika Osaka nchini Japan kuanzia Aprili 12, mpaka 13 Oktoba 2025 huku Wizara,taasisi na sekta binafsi zikitakiwa kujipanga kushiriki.

Amebainisha hayo wakati wa Kikao chake na Waandishi wa Habari kilichohusu ushiriki wa Serikali ya Tanzania kwenye maonesho hayo Aprili 08,2025 Jijini Dodoma.

Waziri Jafo amesema Maonesho hayo yatashirikisha nchi 160 na yanatarajiwa kuwa na watembeleaji Milioni 28.2 ambapo kati ya hawa, watembeleaji Milioni 3.5 watatoka nje ya Japani lengo likiwa ni kutangaza fursa zilizopo.

Dkt.Jafo amesema Siku ya Kitaifa ya Tanzania ni mojawapo ya matukio makubwa yanayoratibwa yatakayofanyika Mei 25,2025 ambapo Nchi itatumia siku hiyo kutangaza fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji, vivutio vya utalii pamoja na mila na utamaduni wa Kitanzania ambapo mgeni rasmi katika maonesho ya Expo 2025 Osaka, ni Waziri Mkuu Kasim Majaliwa.

Aidha amesema Tanzania imejikita kuunganisha uzalishaji wa ndani na masoko ya nje, kuhamasisha Uwekezaji kupitia miradi ya ubia, kuimarisha mawasiliano kati ya watu, bidhaa na teknolojia, kuchochea ujenzi wa miundombinu na kuchochea ukuaji wa Biashara ya Utalii pamoja na kutangaza fursa kwenye sekta mbalimbali.

Alisema katika Maonesho haya Tanzania inatarajia matokeo makubwa katika Kuimarisha intelijensia ya taarifa za biashara zinazowezesha nchi kujipanga na kuzitambua fursa za masoko na Biashara,kuimarika kwa uchumi wa nchi kutokana na matarajio ya kufanikiwa kupata wadau wa miradi mbalimbali ya kimkakati, ajira, Ustawi wa jamii ya Watanzania na Kusainiwa kwa mikataba ya kibiashara na uwekezaji.

Vilevile amebainisha kuwa Programu za kila wiki zimeandaliwa ili kutangaza fursa katika sekta mbalimbali za kiuchumi na zitasimamiwa na Wizara za Kisekta kwa kushirikiana na Taasisi zilizopo chini ya Wizara pamoja na Sekta binafsi huku zikiratibiwa na Wizara ya Viwanda na Bishara pamoja na TANTRADE.