Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

TANZANIA KUENDELEZA USHIRIKIANO NA UTURUKI UWEKEZAJI SEKTA YA VIWANDA ASEMA LONDO


📌Atembelea viwanda kadhaa nchini uturuki kujifunza teknolojia ya viwanda katika maeneo ya uwekezaji;

📌Asema Serikali itaendelea kufungua fursa za kibiashara na nchi za nje kukuza uchumi.


Tanzania na Uturuki zimeeleza utayari wa kuendeleza ushirikiano katika uwekezaji kwenye sekta ya viwanda kupitia timu ya Pamoja ya Serikali za nchi hizo mbili, inayolenga kuangalia fursa zilizopo kwa ajili ya kuendeleza uwekezaji na uzalishaji.

Hayo yamesemwa leo  Oktoba 5, 2026, na  Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, katika Eneo Maalum la Uwekezaji la Şanlıurfa nchini Uturuki, baada ya kupata  fursa ya kutembelea viwanda mbalimbali vilivyopo katika eneo hilo.

Ameeleza kuwa kupitia ziara hiyo wamebadilishana uzoefu wa namna bora ya kusimamia na kuendeleza maeneo maalum ya uwekezaji. Aidha, Mhe Londo alipata nafasi ya kujadiliana na kuwakaribisha kuwekeza kwenye eneo la ujenzi wa viwanda kupitia teknolojia ya prefabricated kwa kutumia saruji, ambazo zinagharama nafuu.

Miongoni mwa viwanda vilivyotembelewa ni kiwanda cha pamba kinachojihusisha na uzalishaji wa nguo, kiwanda cha vifaa vya umeme hasa transfoma, kiwanda cha vyakula na kiwanda cha vifaa vya usalama mahali pa kazi, ambako amepokea maelezo kuhusu shughuli za uzalishaji pamoja na fursa zinazoweza kuunganisha viwanda hivyo na soko na wawekezaji wa Tanzania.

Mhe. Londo amesema ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kutafuta fursa za ushirikiano wa kimataifa zitakazosaidia kuongeza uwekezaji, uzalishaji na kuongeza thamani ya bidhaa, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia uzoefu wa Uturuki katika kuendeleza maeneo maalum ya uwekezaji nchini Tanzania.