Habari
Serikali kuendeleza juhudi za kuboresha na kuimarisha sekta ya viwanda nchini.
Serikali kuendeleza juhudi za kuboresha na kuimarisha sekta ya viwanda nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt.Selemani Jafo (Mb) wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya Wadadisi na Wasimamizi wa Sensa ya Uzalishaji Viwandani kwa Mwaka wa Rejea 2023 Machi 15, 2025 mkoani Iringa.
Dkt. Jafo ameeleza kuwa sensa ya uzalishaji viwandani ni muhimu kwa ajili ya kuandaa mipango ya maendeleo ya kiuchumi, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inajikita katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Lengo kuu la mafunzo hayo imeelezwa kuwa ni kutoa maarifa kuhusu utekelezaji wa sensa ya uzalishaji viwandani kwa mwaka wa rejea 2023, ambapo takwimu zitakusanywa kutoka kwa viwanda mbalimbali vya uzalishaji nchini.
Aidha, imeelezwa kwamba takwimu hizo zitakuwa na manufaa makubwa katika kupanua ufanisi wa viwanda na kuhakikisha kuwa sekta ya viwanda inaongeza mchango wake katika Pato la Taifa.
Mafunzo hayo ya siku 12 yamejumuisha masuala ya mbinu za kukusanya takwimu, kutumia teknolojia katika ukusanyaji wa data, na kutoa maelezo kuhusu umuhimu wa takwimu za uzalishaji viwandani katika kuboresha sera za maendeleo ya kiuchumi.
Naye mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa ameeleza kuwa mafunzo hayo ni mkakati mojawapo wa kuboresha ukusanyaji wa takwimu katika maeneo mbalimbali ili kuwa na Taifa endelevu.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mhe. Kheri James akimuwakilisha Mkuu wa mkoa wa Iringa, amewapongeza wadadisi na wakaguzi waliopata mafunzo hayo ambayo lengo lake ni kujenga nchi bora yenye kufuata taratibu za kitakwimu.