Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Serikali inaendelea kuweka misingi mizuri kwa Wafanyabiashara wazawa nchini ili wafanye biashara vizuri.


Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo (Mb) amesema kuwa Serikali inaendelea kuweka misingi mizuri kwa Wafanyabiashara wazawa nchini ili wafanye biashara vizuri.

Amesema katika Bajeti ya Mwaka huu 2025/2026 imeweka mabadiliko katika kuruhusu biashara kuweza kufanyika na kuzuia wataalam kufunga biashara bila sababu pamoja na badiliko la kuanisha aina ya biashara zitakazofanywa na Wazawa na zile zinazotakiwa kufanywa na wageni ambalo lilikuwa ni shida changamoto kwa muda mrefu.

Dkt.Jafo amebainisha hayo katika Mkutano wa Kumi na Tisa ,Kikao cha 51 Bungeni wakati wa kuchangia hoja kwenye Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 Jijini Dodoma, Juni 23,2025.

Waziri Jafo ameongeza kuwa mabadiliko ya kuanisha Biashara zinazotakiwa kufanywa baina ya wageni na wazawa sio ubaguzi bali hufanyika hata nchi mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha wananchi husika wananufaika ambapo hiyo ni moja ya dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Sulubu Hassan ya kuwasaidia Watanzania.

Aidha Dkt.Jafo amesema katika sera za Dkt.Samia ndani ya Miaka minne Tanzania imetoka kuwa na idadi ya viwanda 52,128 mpaka viwanda 80,128 ambapo eneo hilo linaonesha Tanzania imeanza kujitosheleza katika viwanda kama vile katika viwanda vya bati,Nondo,Sukari na Bati ambapo kwa bati vimeweza kutosheleza mahitaji ya ndani kwani mahitaji ni tani 130,000 na sasa zaidi ya tani 260,000 hivyo ni lazima kulinda.

Vilevile amesema kuwa Taifa litaweka historia katika miradi mikubwa ya vielelezo ya Engaruka na Mchuchuma na Liganga kwani hivi karibuni jiwe la msingi Mradi wa Mchuchuma na Liganga litawekwa ili mradi uanze kazi na kwa upande wa Engaruka taratibu zote zimefanyika hivyo muda simrefu mwekezaji atapatikana kuanza kazi.

Vilevile Dkt.Jafo amewahimiza Watanzania kuhakikisha wanalinda amani ya nchi na wasikubali kuungana na yeyote anayetaka kuhatarisha amani ya nchi.