Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI YAAGIZA FCC NA TBS KUWASHUGHULIKIA WANAOHUSIKA NA BIASHARA HARAMU


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeziagiza Tume ya Ushindani (FCC) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kufanya ukaguzi wa biashara haramu na kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria wahusika watakaobanika.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo katika Hotuba yake iliyosomwa na Kaimu Mkurugenzi wa FCC Bi. Khadija Ngasongwa wakati anamwakilisha katika Warsha ya Uelewa Kuhusu Biashara Haramu iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es salaam iliyoandaliwa na Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) Agosti 25,2025.

Akisoma hotuba hiyo Bi. Khadija amesema serikali imekadiria kupoteza kiasi cha shilingi Bilioni 16.53 kwa mwaka kutokana na biashara haramu ya Sigara ambapo hadi mwisho wa mwaka 2025 kiasi cha shilingi Bilioni 18 kitakuwa kimepotea ikiwa hatua haitachukuliwa.

Aidha Bi. Khadija amesema uchumi wa Tanzania unaathiriwa kutokana na biashara haramu inayosababisha kupotea kwa mapato yatokanayo na ukwepaji wa kodi kwa sababu ya kupotosha bei za soko, kusababisha ushindani usio wa haki na kudhoofisha viwanda vya ndani.

Vilevile Bi. Khadija amezitaka taasisi hizo kuendelea kutoa elimu zaidi kwa Watanzania ili kuwapa uelewa kuhusu athari za biashara haramu na kuwaomba wananchi kuwa na utamaduni wa kununua bidhaa halali na kudai risiti za EFD ili kuhakikisha ulipaji wa kodi na kujenga uchumi wa Tanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Biashara Bw.Sempeho Manongi kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt.Hashil Abdallah ameagiza kutafutwa na kuvunjwa kwa mitandao ya biashara haramu ya Sigara ili kulinda Viwanda vya ndani.

Sempeho amesisitiza kuwa biashara hiyo ni kosa la kimtandao na linahitaji mshikamano wa wadau wote wa Kisekta ili kukabiliana na tatizo hilo na kuahidi kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara itatoa ushirikiano wa kutosha kupambana na biashara hizo haramu.