Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Serikali Kupitia sera mpya ya biashara imelenga kupanua wigo wa masoko na kuwawezesha wajasiriamali


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt. Selemani Jafo amesema Serikali Kupitia sera mpya ya biashara imelenga kupanua wigo wa masoko na kuwawezesha wajasiriamali hususani wanawake kufikia masoko kwani Tanzania ina fursa ya kuuza bidhaa zake zaidi ya nchi 50 barani Afrika.

Amesema katika juhudi za kuwaendeleza kina Wanawake kufikia masoko hayo wizara imeweka utaratibu maalum wa kuwaunganisha na taasisi kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ambalo litawalea kwa kipindi cha miaka mitatu bila malipo hatua ambayo inalenga kuwasaidia wanawake kuingia sokoni na bidhaa zenye ubora unaokidhi viwango vya kimataifa.

Dkt.Jafo amebainisha hayo Katika uzinduzi wa Women Health Package kwa kushirikiana na Integrated Empowerment Initiative (IEI) na Women Tapol Machi 7,2025 Jijini Dar es Salaam.

Aidha, Dkt. Jafo amesisitiza mshikamano na upendo miongoni mwa wadau wa sekta ya biashara ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana pamoja na wadau mbalimbali kushirikiana na serikali katika kuwawezesha wajasiriamali wadogo ili kuimarisha biashara zao.

Vilevile Dkt.Jafo amepongeza maboresho ya miundombinu ambayo yamechangia kukuza uchumi, kurahisisha upatikanaji wa bidhaa, na kuwezesha biashara kati ya Tanzania na mataifa mengine.