Habari
Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) na Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) ina teknolojia ya kuchakata migomba
Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) na Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) ina teknolojia ya kuchakata migomba kwa ajili ya chakula cha mifugo na viwanda vya kutengeneza mvinyo, unga wa lishe, keki na crisps zinazotokana na ndizi.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb) ameyasema hayo Aprili 10, 2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Buhigwe Kavejuru Eliadory ambapo ameuliza,
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Viwanda vya kuchakata zao la Migomba?
“Mheshimiwa Spika, Kwa kutambua umuhimu wa uongezaji thamani zao la migomba pamoja na ndizi, Serikali kupitia SIDO imepanga kuanzisha Kongani ya zao la migomba/ndizi katika Halmashauri ya Buhigwe”, amesema.
“Mpango huo unatarajiwa kuanza ifikapo Julai, 2025 kwa majadiliano kati ya SIDO na Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe ili kukubaliana eneo ambalo Kongano hiyo itawekwa pamoja na gharama za programu hiyo”. Amesema Kigahe
Vilevile amesema Kutokana na tafiti zilizofanywa duniani, zao la migomba lina faida nyingi ikiwa ni pamoja na kutumika kutengeneza bidhaa za asili kama vile vikapu, mikeka na kofia.
“Zao hilo hutumika kutengeneza chakula cha mifugo, mbolea, nguo, karatasi, nishati ya kupikia, dawa za asili na malighafi za kujengea”, amesema
“Hivyo, zao hili ni miongozi mwa rasilimali zinazopatikana nchini zitakazoongezewa thamani kupitia Mpango Maalum wa Kuendeleza Viwanda wa Miaka Mitano (5) unaotarajiwa kutekelezwa kuanzia Mwaka wa Fedha 2025/26 hadi 2029/30”. Amesema Kigahe