Habari
Serikali kuendelea kuwasaidia wajasiriamali kukua kibiashara zaidi.
Serikali kuendelea kuwasaidia wajasiriamali kukua kibiashara zaidi.
Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe.Exaud Kigahe (Mb) amesema Serikali itaendelea kuwasaidia wajasiriamali kukua na kuendelea kuwa shindani ili waweze kuzalisha kwa tija wauze kwenye masoko ya ndani na nje.
Mhe. Kigahe ameyasema hayo Machi 3,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa maonesho ya wanawake na vijana yaliyoandaliwa na Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC).
Taasisi 13 zilizopo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, zipo kwaajili ya kurahisisha fursa ya kibiashara ili zikubalike ndani na nje ya nchi.
Amesema hatua hiyo pia itaongeza ajira kwa vijana na kinamama na kupata fedha za kigeni pamoja na kupunguza uingizwaji wa bidhaa ambazo zinaweza kuzalishwa hapa nchini.
“Maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kwamba tuhakikishe sekta binafsi inakuwa ndiyo sekta kiongozi katika kufikia lengo la kuwa na uchumi wa kati, daraja la juu, jumuishi na viwanda. Kote duniani wajasiriamali ndio ambao wanazalisha kwa wingi bidhaa mbalimbali ambazo nyingine ni za mwisho kwa sababu zinakwenda kwa walaji lakini nyingine ni za kati ambazo zinakwenda kwenye viwanda vya juu.
“Ombi langu kwa wajasiriamali tuendelee kutumia fursa nzuri ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ameweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara hapa nchini, taasisi zetu ambazo ziko chini ya wizara na zingine za serikali ziwasaidie wajasiriamali kukua, wafanyabiashara kufanikiwa, kuendelea na kuwa shindani ili waweze kuzalisha kwa tija na kwa ubora waweze kuuza kwenye masoko ya ndani na washindi.
Mhe. Kigahe amewahakikishia wajasiriamali wanawake, vijana na Watanzania wote kwamba Serikali ipo nao bega kwa bega na itahakikisha wanatimiza malengo yao na kuwa chachu ya maendeleo ya nchi.
Aidha, ameipongeza TWCC kwa kuandaa maonesho hayo na kuahidi kuwa kama wizara yenye dhamana hawatawaacha nyuma kwa kuwa wanawajali wajasiriamali.
Naye Rais wa TWCC,CPA(T) Mercy Sila, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini.
“Sisi ni wanawake lakini tuko na vijana, tumefungua dirisha la vijana wavulana wako ili wote kwa pamoja tujenge nchi yetu,” amesema